Ziara hii iliyoratibiwa na Mradi wa HEET iliwawezesha Wanafunzi wa Shahada ya Awali ya Sayansi ya Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda wa Chuo Kikuu Mzumbe, tarehe 25 April 2024 kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo yale waliojifunza darasani walipofanya ziara ya mafunzo katika kiwanda cha kusindika matunda cha Azam Bakhresa kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Msimamizi wa Udhibiti bora katika kiwanda hicho Bw. Ibwa E. Backita amesema, “Kiwanda cha Bakhresa kinazalisha vinywaji vya kaboni (soda) ice cream, maji na kuchakata matunda (juisi).
Akielezea namna gani kinywaji aina ya soda kinavyozalishwa kiwandani hapo hatua kwa hatua Bw. Ibwe alisema, “lazima kuwe na maji safi na salama, Acid ya citric, sukari nyeupe na viungo, (flavor)”
Bw. Hemed Abdallah, Mtaalamu wa udhibiti bora alisema mitambo inayotumika ni ya kisasa na malighafi zenye ubora kwa kiwango cha juu (ISO Standard).
Pia, wanafunzi walipata fursa ya kuona kwa vitendo jinsi soda zinavyozalishwa hatua ya kwanza mpaka pale inapomfikia mlengwa.
Akishukuru kampuni ya Bakhresa Food Product, Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Doya Ndaria kutoka idara ya Sayansi ya Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda amesema dhumuni la ziara hiyo ni kuwawezesha wanafunzi kuhusianisha nadharia za darasani na uhalisia katika maeneo ya kazi ambayo itawasaidia kujiajiri.