Na Dk. Reubeni Lumbagala
Ummy Ally Mwalimu ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aliingia bungeni mwaka 2010 kwa mwamvuli wa viti maalum hadi mwaka 2020. Ilipofika mwaka 2020 aliamua kugombea jimbo la Tanga Mjini ambapo aliibuka kidedea na kufanikisha kuwawakilishi wananchi katika jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano yaani 2020-2025.
Moja ya ahadi ya Mbunge Ummy kwa wananchi wake ni kuhakikisha wafanyabiashara wa Tanga Mjini wanafanya biashara zao katika mazingira mazuri na rafiki ili kukuza uchumi wao na wa Taifa. Masoko ni moja ya eneo ambalo lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi.
Kutokana na ukweli huo, Mbunge Ummy Mwalimu ameipa nguvu na msukumo mkubwa sekta ya masoko ili wananchi wa Tanga Mjini waweze kunufaika na hatimaye kuboresha hali zao za kiuchumi.
Jimbo la Tanga Mjini lina masoko mengi, mathalani soko la Uzunguni, Kisosora, Majani Mapana, Makorora, Mgandini, Ngamiani, kutaja kwa uchache ambayo yanachangia sana kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri na ya nchi pia kupitia ushuru na kodi zinazolipwa na wafanyabiashara.
Ili kuongeza hamasa kwa wafanyabiashara kulipa ushuru na kodi kwa hiari, mazingira wanayofanyia biashara yanapaswa kuboreshwa na kuwa bora zaidi ili wafanyabiashara waone tija ya kuendelea kulipa kodi serikalini.
Inapotokea wafanyabiashara wanalipa kodi zao, lakini hakuna uboreshaji wa mazingira yao ya kufanyia baishara, wanavunjika moyo wa kuendelea kulipa kodi na hvyo kuilalamikia serikali yao kwa kushindwa kuwahudumia ipasavyo.
Kutokana na umuhimu wa uboreshaji wa mazingira ya wafanyabishara wakiwemo wa masokoni, Mbunge Ummy Mwalimu amefanya juhudi kubwa za kuboresha mazingira ya masoko kwa kuhakikisha masoko ya Tanga Mjini yanaboreshwa na kuwa ya kisasa zaidi ili kuchochea uchumi wa wananchi na Taifa.
Serikali ilibuni mradi wa uendelezaji miji kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), mradi huo unajulikana kwa jina la Green & Smart Cities. Mradi huu unazinufaisha majiji ya Tanga, Mwanza na Halmshauri ya Ilemela.
Kwa Tanga Jiji, mradi huo utakuwa na manufaa kwa kuwa utajenga masoko ya kisasa ya vyakula kutoka mashambani, soko la uchakataji wa samaki, miundombinu ya kijani, kudhibiti maji taka, kuboresha maji safi na kuhakikisha taka zote zinzozalishwa jijini Tanga zinachakatwa na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Sekta ya masoko katika jimbo la Tanga Mjini itanufaika moja kwa moja kwani kupitia mradi wa Green & Smart Cities utaboresha masoko matatu ya Mlango wa Chuma, Mgandini na lile la Samaki Kasera. Katika Bajeti ya 2024/2025, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) imeshaidhinisha utekelezaji wa miradi huu. Kwa mantiki hiyo, kuanza kwa bajeti mpya Julai Mosi, 2024, kunatoa fursa ya ujenzi wa masoko hayo matatu ambayo kwa pamoja yatagharimu shilingi bilioni 52.5 ambayo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Mbunge Ummy Mwalimu kwa wananchi wake wa Tanga Mjini kuinua sekta ya masoko.
Kutokana ya masoko haya kujengwa kisasa na kuwa makubwa kuliko ilivyo sasa, kunatoa fursa kwa wafanyabiashara wengi kupata vizimba vya kufanya biashara kuliko idadi ya sasa. Ongezeko la wafanyabiashara katika masoko haya matatu kunaongeza ajira kwa wananchi na hivyo kuboresha uchumi moja kwa moja.
Vilevile, masoko haya yataongeza makusanyo ya ushuru na kodi kutoka kwa wafanyabiashara. Mradi wa masoko haya matatu yanategemewa kuongeza makusanyo na hivyo kuimarisha mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Tanga na nchi kwa ujumla.
Kuinua sekta za kilimo na uvuvi. Masoko haya yatakuwa chachu kwa wakazi wa mkoa wa Tanga kuongeza uzalishaji katika kilimo na uvuvi kwani kutakuwa na masoko ya uhakika kwa ajili ya mazao ya kilimo na uvuvi. Ikumbukwe kilimo na uvuvi ni sekta muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Tanga. Ujio wa masoko haya ya kisasa ya Mgandini,
Mlango wa Chuma na Samaki Kasera, kuna mchango wa moja kwa moja katika kuinua kilimo na uvuvi.
Pamoja na hayo, pia masoko haya yatakuwa chachu ya uboreshaji wa sekta nyingine kama vile elimu, afya, maji, miundombinu. Mafanikio ya sekta moja yanagusa pia sekta nyingine.
Ongezeko la mapato kutokana na masoko haya, yataijengea uwezo wa kimapato Halmashauri ya Jiji la Tanga na hivyo kuwa na kumudu kuboresha sekta hizo kupitia mapato ya ndani na hivyo kuchochea maendeleo zaidi kwa wakazi wa Tanga na Taifa kwa ujumla.
Ni muda muafaka sasa kwa wakazi na wananchi wa Jiji la Tanga kuchangamkia fursa ya vizimba katika masoko haya matatu pindi yatakapokamilika ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wao. Halmashauri ya Jiji la Tanga iendelee kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha masoko mengine ili kukuza biashara.
Mbunge Ummy Mwalimu aendelee kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuboresha zaidi masoko jijini Tanga ili kuchagiza zaidi maendeleo ya wapiga kura. Kwa hakika, masoko yote Tanga Mjini yakiboreshwa na kuwa ya kisasa, yatasaidia sana kuboresha hali za kiuchumi za wananchi wa Tanga. Juhudi zilizofanywa na Mbunge Ummy Mwalimu za kuinua sekta ya masoko Tanga Mjini ninapaswa kuungwa mkono na wananchi kwa kuchangamkia fursa hiyo muhimu ya kiuchumi.
Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.