Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud
akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati
alipotembelea taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma za
matibabu ya moyo zinazotolewa.
Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akisaini
kitabu cha wageni wakati alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo
kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akiangalia
video fupi inayoonesha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona huduma za
matibabu ya moyo zinazotolewa.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akimwelezea Rais wa Jamhuri
ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud kuhusu huduma ya upasuaji mdogo wa
moyo inayotolewa katika mtambo wa Cathlab wakati Rais huyo alipotembelea leo
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud akiwa
katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
mara baada ya kumaliza ziara yake ya kuona huduma za matibabu ya moyo
zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge akimweleza Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh
Mohamud huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na Taasisi hiyo wakati Rais
huyo alipotembelea Taasisi hiyo.
…………………….
27/4/2024 Rais wa Jamhuri ya Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud amewapongeza wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma nzuri wanayoitoa ya kuokoa maisha ya watu wenye matatizo ya moyo.
Mhe. Rais Hassan Sheikh Mohamud alizitoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Akiwa katika Taasisi hiyo Mhe. Rais Mahamud alitembelea maeneo mbalimbali ya JKCI ikiwa ni pamoja na mtambo wa Cathlab ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwaajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI ni moja ya Taasisi inayoongoza katika nchi za Afrika Mashariki na kati katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Dkt. Kisenge alisema Rais Mohamud alitembelea Taasisi hiyo kwaajili ya kuona namna ambavyo nchi ya Somalia itawapeleka wagonjwa wa moyo JKCI kupata tiba ya matibabu ya moyo.
“Nchi ya Somalia inawapeleka wagonjwa wengi wa moyo kwenda kutibiwa katika nchi za India, Ulaya na Marekani wakati huduma hii inapatikana nchini Tanzania, na ukiangalia nchi hizi ziko karibu hivyo basi itakuwa ni rahisi kwao kuwaleta wagonjwa kuja kutibiwa hapa kwetu”.
“Kuja kwa wagonjwa hawa kutaisaidia nchi yetu kukua kiuchumi kwani pesa zitakazopatikana zitawafikia watu wengi ikiwemo wamiliki wa hoteli ambako wagonjwa watalala pamoja na wafanyabiashara watakaowauzia vyakula na mahitaji mengine”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alimshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzidi kuimarisha mahusiano na nchi za nje ndiyo maana watu wengi wanakuja kuwekeza hapa nchi hata Taasisi hiyo imekuwa ikiwapokea wageni mbalimbali kutoka nchi za nje.
Akiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mhe. Rais Hassan Sheikh Mohamud pamoja na ujumbe wake aliambata na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu.