Na Sophia Kingimali.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanafuatilia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea katika kipindi hiki cha mvua huku serikali ikiwa enaendelea kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika.
Wito huo ameutoa leo wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uwanja wa Uhuru yaliyohudhuriwa na Marais kutoka nchi mbalimbali Afrika.
“Serikali inafanya kila linalowezekana ili kurejesha miundombinu iliyoharibika na leo hapa nimealika benki ya dunia kwa madhumuni maalum kabisa najua tutapata pesa ya kurejesha miundombinu yetu”Amesema Dkt Samia.
Aidha Dkt Samia amewataka Watanzania kuendelea kuuenzi Muungano kwa kufanyakazi kwa bidii na kudumisha ushirikiano kwa kutunza amani.
Amesema Muungano umetokana na sisi wenyewe hivyo tunapaswa kuendelea kuutunza ikiwa kama sehemu ya kuwaenzi waasisi wa Muungano wetu.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amesema maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwani yamekuwa na vionjo vingi ikiwemo uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Naye,Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupata sifa kimataifa na kuwa mfano kwa nchi jirani kwa mshikamano na amani iliyopo.
“Ni jambo la faraja kuona mambo mengi ya muungano yameshapatiwa ufumbuzi hivyo tunaahidi kuuenzi na kuendelea kuuenzi na kudumisha muungano wetu”,Amesema.
Nao Marais walioshiriki kwenye maadhimisho hayo wamesema Tanzania imekuwa nchi ya mfano wa kuigwa kwa Muungano na ushirikiano walionao kwani umepelekea nchi hiyo kuwa na Amani.
Maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu 2024 yameadhimishwa kwa namna ya kipekee kwani kumekuwa na matukio mbalimbali yakiwemo uzinduzi wa miradi ya kimaendeleo ambapo kauli mbiu inasema ‘Tumeshikamana na Tumeimarika kwa maendeleo ya Taifa letu’