Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala amewaongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Manyara kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
DC Lulandala ambaye amemwakilisha Mkuu wa mkoa huo Queen Cuthbert Sendiga amewaongoza wana Manyara kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika mji mdogo wa Orkesumet.
DC Lulandala akizungumza kwenye maadhimisho hayo amesema miaka 60 ya muungano imekuja na mafanikio mengi mkoani Manyara.
Lulandala amesema miaka 60 ya muungano imekuwa na maendeleo makubwa mkoani Manyara, hususani kwenye sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.
“Mkoa wa Manyara umekuwa na mafanikio makubwa katika miaka 60 ya muungano na wananchi wanaona kwa macho maendeleo mengi yaliyofanyika,” amesema DC Lulandala.
Amesema kwenye wilaya ya Simanjiro kumekuwa na mafanikio mengi ikiwemo vijiji vyote 56 kupata nishati ya umeme kwani vijiji 35 vilivyobaki vilifungiwa kwa miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, awali vilikuwa vijiji 21.
Katibu Tawala wa Mkoa RAS wa Manyara, Maryam Ahmed Muhaji amesema miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar imezidi kuwa na mshikamano kwa watanzania hivyo wataendelea kuuenzi.
Makamu Mwenyeki wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza nchi kwa miaka mitatu akifuata misingi, falsafa na maono ya waasisi wa Taifa hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Abeid Amani Karume. amesema.
Katibu Tawala wa wilaya hiyo, DAS Warda Abeid Maulid amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kuhudhuria kwa wingi katika maadhimisho hayo.
Meneja wa shirika la ugavi wa nishati (TANESCO) wilayani Simanjiro, Sixmund Mosha amesema tarafa zote sita, kata zote 18 na vijiji vyote 56 vimepata nishati ya umeme.
“Hivi sasa kazi ya kufunga nguzo na vifaa vingine inaendelea ili kumaliza vitongoji vyote 278 viwe na umeme kwani Simanjiro ni kubwa yenye kilomita za mraba 29,591,” amesema meneja Mosha.
Mfugaji wa kata ya Orkesumet wilayani Simanjiro, Mokia Mirimba amesema wafugaji wengi hivi sasa wamenufaika kiuchumi na kupiga hatua.
Mirimba amesema wafugaji wameweza kupata mikopo ya riba nafuu kupitia taasisi za fedha na kunenepesha mifugo hivyo kujinufaisha kiuchumi.
“Hivi sasa wafugaji tunatambulika na taasisi za fedha hivyo tunakopesheka tofauti na awali na kusababisha kunufaika kiuchumi na kupiga hatua ya maendeleo,” amesema Mirimba.
Mfugaji wa kata ya Langai Sarah Elifuraha amesema miaka 60 ya muungano imewanufaisha wafugaji kwani wamepatiwa mikopo ya asiimia 10 ya mapato ya ndani halmashauri.
“Wafugaji tunazidi kupiga hatua ndiyo maana leo tupo kifua mbele kuadhimisha miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” amesema.
