………………………..
NA MUSSA KHALID
Wanamuziki wa Reggae nchini na Maeneo ya Ukanda ndani ya Bara Afrika wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Tuzo za Muziki wa Reggae za KMCC Reggae Music Awards (KRMA III) zinazotarajiwa kufanyika Julai mosi mwaka huu.
Akizungumza wakati wa utambulizo wa ujio wa Tuzo hizo kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mwakilishi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Abel Ndaga ameipongeza Taasisi ya KMCC kwa kuandaa Tuzo hizo kwani zitaendelea kuongeza hamasa kwa wasaini nchini wa Reggae nchini hivyo kukuza Muziki huo.
Aidha amevitaka vyombo vya habari na wadau mbalimbali Nchini wakiwemo wanamuziki wa Reggae kuonyesha ushirikiano katika kuhamasika kushiriki katika mchakato huo ikiwemo kushirikisha kazi zao za muziki ili ziweze kushindanishwa na hatimaye kujipatia zawadi.
“Sisi kama BASATA tutaendelea kuwaunga mkono wasanii na taasisi mbalimbali katika mipango yao mbalimbali wanayoipanga kwa lengo la kukuza vipaji vya wasanii nchini”amesema Ndaga
Akitambulisha ujio wa Tuzo hizo Mratibu wa Taasisi ya Kukaye Moto Culture Center (KMCC-Tanzania) Diana Martin amesema kuwa Tuzo hizo ni miongoni mwa miradi ya KMCC ambazo mwaka huu zinafanyika kwa mara ya Tatu ukiwa ni msimu ulioboreshwa zaidi.
Diana amesema kuwa Tuzo hizo zimelenga kutambua mchango adhimu wa muziki wa Reggae kwa jamii na mchango muhimu kwa wanamuziki wa Mtindo huu hapa nchini ili kuwahamasisha kwa kutambua na kuthamini wanachokifanya.
“Tuzo hizi zinaongozwa na mchakato ulioundwa na Kamati ya Weledi zimezingatia ithibati ya Mamlaka simamizi (BASATA),COSOTA na kushirikisha washiriki na wadau kupitia Taasisi zao (BOREDA & RUF) katika hatua za mchakato Ili kuwa na ushirikishanaji Jumuishi utakaojenga ushirikiano miongoni mwa Wana-Reggae nchini”amesema Diana
Aidha kuhusu Mchakato,Diana amesema kuwa ulianza rasmi Januari 27 ambapo unatarajiwa kukamilika Juni 30 kilele cha Usiku wa utoaji Tuzo husika Kuamkia siku ya maadhimisho ya Reggae Duniani Julai Mosi.
Diana amesema kuwa katika Tuzo hizo vipengele mbalimbali vya Muziki wa Reggae visivyopungua thelathini na mojavitatuzwa zikiwemo kazi (Nyimbo) Bora na wasaini waliofanya vizuri zaidi mwaka 2023 kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo za KRMA III Innocent Nganyagwa maarufu Ras Inno ametaja mchakato wa huo kuwa umezingatia zaidi ya vipengele 30 vitahusika ambapo pia utafanyika uchakataji wa kazi pamoja na upatikanaji wa wateule.
‘Matarajio yetu ni Ushiriki wa Wasanii wa Reggae na kuwa na mwamko wa Hadhira kushiriki sambamba na hatua ya awali ya kusadifisha Muundo (KRMA IV na kuendelea)’amesema Ras Inno
Amevitaja vipengele mbalimbali vitakavyoshindaniwa kuwa ni pamoja na Mwanamuziki Bora wa Kiume wa Dancehall wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Kike wa Dancehall wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Kiume wa Reggae wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Kike wa Reggae wa Mwaka, Wimbo Bora wa Reggae wa Mwaka, Wimbo Bora wa Dancehall wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Reggae/Dancehall wa Kiume wa Mwaka Anayechipukia, Mwanamuziki Bora wa Reggae/Dancehall wa Kike wa Mwaka Anayechipukia, Wimbo Bora wa Kushirikisha/Kushirikiana wa Reggae/Dancehall wa Mwaka, na Mnenguaji Bora wa Video wa Kiume wa Dancehall wa Mwaka:
Pia amevitaja vipengele vingine kuwa ni Albamu Bora ya Reggae ya Mwaka, Video Bora ya Reggae ya Mwaka, Mtunzi Bora wa Reggae wa Mwaka, Mtunzi Bora wa Dancehall wa Mwaka, Mwanamuziki Bora wa Reggae/Dancehall wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Mwanamuziki Bora Dancehall/Reggae wa Ukanda wa Afrika ya Kusini, Mwanamuziki Bora wa Reggae/Dancehall wa Kaskazini mwa Afrika.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Reggae na Dancehall (BOREDA) Grant Cosmas maarufu kama Sukuma Di Push amesema watahakikisha wanakuwa bega kwa bega na KMCC katika Tuzo hizo ili ziweze kuwa na ukubwa zaidi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Rastafari United Front Ras Mabondo Makonnen ameendelea kusisitiza Umoja na upendo kwa jamii ya Rasta huku akielezea kuwa ujio wa Tuzo hizo utasaidia kuongeza wigo wa kukuza mawanda ya Muziki huo hapa nchini.