NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI mkoani Mwanza imefarijika viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),kukutanishwa na viongozi wa Serikali ngazi mbalimbali na kupata pamoja taarifa na takwimu za mawasiliano.
Pia,imeziagiza taasisi mbalimbali za umma zijifunze kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF),kushirikisha wadau zinapoandaa mikutano yao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda, leo alipozindua kampeni ya elimu kwa umma mkoani humu kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano nchini.
Amesema UCSAF kukutanisha viongozi wa Chama na Serikali pamoja kupata takwimu za miradi ya mawasiliano ni jambo la kuigwa na taasisi zote za umma zinapoandaa mikutano yao mkoani Mwanza, ili kupata uelewa wa pamoja.
“Sisi kama makamisaa tumefarijika sana ma azma yetu ni kuhakikisha tunaendelea kushika dola, haiwezekami kushika dola bila mawasiliano ya uhakika.Mtakumbuka tunaelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2025, hivyo ni lazina kuwe na mawasiliano imara ya uhakika ”alisema Masala.
Mkuu huyo wa Wilaya ametumia fursa hiyo kuziagiza taasisi zote za serikali mkoani humu,zinapoandaa mikutano yao zijifunze kupitia mfuko wa UCSAF kuwashirikisha viongozi wa Chama na Serikali.
“Naamini wakuu wa wilaya,maofisa tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti wa halmashauri na madiwani mliohudhuria kampeni hii ya elimu kwa umma kuhusu utekelezaji mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, mtakwenda kwa wananchi kukisemea Chama Cha Mapinduzi na Serikali vizuri,”amesema Masala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega amesema vita iliyopo duniani kwa sasa ni teknolojia,serikali kujenga minara yake ni kuhakikisha ulinzi wa mitandao ya kijamii unaimarika.
“Ujenzi wa minara 758 ni jambo zuri,changamoto ni gharama kubwa za simu hasa za kisasa,zikiuzwa kwa bei ya chini wananchi wengi watanunua na serikali itapata mapato,”almesema Bega.
Ameishauri serikali uangalia na ku-regulaty (kusimamia) bei za vifaa vinavyotumia mawasiliamo ya minara inayojengwa na serikali kwa ubia na sekta binafsi ili kuwezesha wananchi kumudu gharama za kununua vifaa hivyo.
Naye Joseph Mazura wa Tarafa ya Mmbuga wilayani Ukerewe, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, licha ya mnara kuwashwa eneo la Bukwimwi bado kuna changamoto ya mawasiliano hafifu.
Changamoto nyingine ya ukosefu wa huduma ya mawasiliano inakikabili kisiwa cha Gana kinachokaliwa na jamii ya wavuvi,wanakosa huduma hiyo baada ya saa 6 wanaposafiri kutoka Ukerewe hadi kisiwani hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Johari Samizi amehoji kuwa mkoani Mwanza,imejengwa minara 16, mmoja tu umewashwa lini iliyobaki itawashwa wananchi wapate huduma.