Na Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma
KESHO kutwa Aprili 26, 2024 inatimia miaka 60 tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuunda Jamhuri Muungano wa Tanzania. Kwa hakika tuna kila sababu ya kujivunia muungano huu ambapo umedumu kwa miaka miaka 60 sasa.
Kwa sheria za kazi na utumishi wa umma, mtu mwenye umri wa miaka 60 anapaswa kustaafu kazi. Hivyo miaka 60 si haba, ni umri wa mtu mzima ambaye sasa anaingia kwenye uzee.
Waasisi wa muungano huu Hayati Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanganyika na Hayati Abeid Amani Karume kwa upande wa Zanzibar ambao kwa pamoja walikubaliana kuziunganisha nchi zao na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo walichanganya udongo kutoka pande zote kama ishara ya muungano.
Kutokana na raia wa pande zote mbili kuwa ni waafrika, nchi hizi mbili kuwa karibu kijiografia (Geographical closeness), kuongea lugha moja ya Kiswahili, kufanana tamaduni kwa kiasi kikubwa, urafiki wa Hayati Nyerere na Karume, Kufanana itikadi kwa vyama viwili vya Tanganyika African National Union (TANU) kwa upande wa Tanganyika na Afro Shirazi Party (ASP) kwa upande wa Zanzibar na kufanana historia, waasisi hawa waliona ni jambo jema kuungana.
Mchambuzi wa siasa na Diplomasia, Abbas Mwalimu anasema udugu wa watu wa Tanganyika na wa Zanzibar ulianza tangu karne ya 12, kipindi ambacho hata mwasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwa amezaliwa wala Skeikh Abeid Aman Karume.
Anasema udugu huu unaweza kuonekana katika sura ya maeneo ambayo mara nyingi watu huwa na kawaida ya kuhama na majina ya maeneo yao. “Kwa mfano ukitoka leo ukaenda Msumbiji utakutana na eneo linaitwa Pemba.
Lile eneo ukiangalia asili yake utaona Wazanzibari wengi walifanya biashara eneo lile na hata kwenye Muungano ukitoka Dar es Salaam ukienda Zanzibar utakutana na sehemu inaitwa Magomeni. Hii inaonesha hawa walikuwa ndugu.
Kinachowatenganisha ni jiografia tu. Pia ukienda maeneo ya Mbweni nayo utakutana nako kuna Zanzibar vilevile, Kariakoo ukienda Zanzibar utaikuta na ukienda Pongwe, kuna Pongwe ya Bagamoyo na Pongwe ya Tanga na ukienda Zanzibar Kaskazini Unguja unaikuta Pongwe.
Sasa unaweza kuona kwanini majina haya yanashabihiana, hii inakupa picha kuwa hawa walikua ndugu lakini wakagawanywa na sababu za kijiografia,” amefafanua Abbas Mwalimu akizungumza katika Studio za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Mchambuzi huyo anasema nchi mbalimbali zimejaribu kuungana lakini muungano wao ni tofauti na wa Tanzania kwa kuwa Tanzania muungano wake ni baina ya watu na si maeneo na ndio sababu hauitwi Jamhuri ya Muungano ya Tanzania bali Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Neno ‘wa’ likiwakilisha watu na sio ‘ya’ ambayo ingewakilisha maeneo.
Manufaa ya muungano wetu yanagusa mambo mengi kuanzia masuala ya kisiasa, kiusalama, kijamii na kiuchumi na hivyo kuwa na kila sababu ya kuendelea kuimarisha muungano huu na kuepukana na chokochoko zote zinazowekaza kuhatarisha kuhatarisha ustawi wake.
Amani na mshikamano wa kitaifa umeendelea kuimarika sana katika miaka hii 60 ya muungano. Viongozi na wananchi wa pande zote wameendelea kuheshimiana na kulinda na kuhakikisha amani iliyoasisiwa na waasisi wa muungano huu inaendelezwa kikamilifu.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa pamoja wamekuwa vielelezo katika kuhakikisha amani na mshikamano wa kitaifa unaendelezwa ili wananchi waendelee kunufaika na muungano huu.
Aidha, muungano umeendelea kuwa nyezo muhimu ya kuimarisha udugu wa damu kwa wananchi wa pande zote mbili. Wananchi wote wamekuwa ni ndugu sasa bila kubaguana. Aidha, muungano umesaidia kuchangamana kwa wananchi na hivyo kuoana na kuzaliana.
Hii imesaidia sana wananchi kuwa kitu kimoja kupitia kuoana na kuzaliana na kuondoa kabisa suala la ubaguzi. Muungano huu sasa si wa kuchanganya udongo bali kuchanganya damu.
Muungano umesaidia sana kuimarisha suala la ulinzi na usalama. Waasisi wa muungano wetu walidhamiria kusaidiana katika suala la ulinzi na usalama kwani ulinzi na usalama ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.
Hivi karibuni, akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango aligusia suala la usalama akisema baada ya Sultani aliyekuwa akitawala Zanzibar kutimuliwa, kulikuwa na tetesi ya kujipanga upya kurejea kivita na kupiga hadi Tanganyika na hivyo muungano ulikuwa muhimu kwa usalama wa pande zote za muungano. Ni katika muktadha huo, tumeshuhudia miaka 60 yenye mafanikio ya ulinzi na usalama.
Wananchi wameendelea kufanya shughuli zao za uzalishajimali kwa uhuru mkubwa kutokana na kuimarika kwa ulinzi na usalama.
Vyombo vya ulinzi na usalama kutoka pande zote wamekuwa wakishirikiana sana kuhakikisha ulinzi na usalama unaendelea kuwepo siku zote.
Muungano pia umekuwa na mafanikio kwa upande wa uchumi kutokana na uhuru uliopo wa raia kutoka pande wote mbili kufanya shughuli za kiuchumi na kibiashara ili kuongeza pato lao na nchi kwa ujumla.
Mwananchi kutoka Tanzania bara yuko huru kufanya shughuli za kiuchumi Zanzibar na kinyume chake ili mradi afuate taratibu na sheria zinazoongoza kufanya shughuli hizo za kiuchumi na kibiashara.
Muungano vilevile umetoa uhuru kwa wananchi kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi, mathalani; kilimo, uvuvi, ufugaji, usafirishaji, madini, nishati na huduma mbalimbali za kijamii.
Uhuru huu umewezesha wananchi kuwekeza katika shughuli hizo na kukuza uchumi.
Wananchi pia kupitia muungano wamenufaika kwa kuwa huru kutumia raslimali zinazopatikana mathalani ardhi na bahari katika shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya. Aidha, muungano umesaidia kukuza sekta za utalii, uvuvi na uchumi wa buluu kwa kiwango kikubwa kwa pande zote mbili.
Nihitimishe makala haya kwa kusema, kutokana na manufaa mengi ya muungano, wananchi wa pande zote mbili tuna kila sababu ya kuendelea kudumisha muungano huu kwa nguvu zetu zote.
Tunahitajiana sana kuliko wakati wowote katika historia ya nchi zetu hizi mbili. Juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wa pande zote mbili za kukuza maendeleo zitaendelea kuzaa matunda zaidi endapo tutaendelea kudumisha muungano huu.
Kwa hakika tumeshikamana na tumeimarika sana katika miaka 60 ya muungano na ndiyo maana tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo ambazo kila mwenye macho anajionea mwenyewe.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni : 0620 800 462.