Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuziunganisha kodi ya jengo na kodi ya ardhi.
………………….
Na. Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa inaandaa mfumo wa kielektroniki wa kutoa ankara ya pamoja kwa huduma zinazolandana ili kuondoa usumbufu kwa wananchi wanaostahili kulipa kodi ya jengo na kodi ya ardhi.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuziunganisha kodi ya jengo na kodi ya ardhi.
“Serikali kupitia Kamati ya Moberesho ya Mfumo wa Kodi inaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya mifumo ya kodi, ada na tozo za huduma kwa lengo la kuondoa urasimu na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini”, alisema Mhe. Chande.
Alisema tathmini hiyo inajumuisha mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa usimamizi wa kodi ya jengo na kodi ya ardhi kama inavyopendekezwa na Mheshimiwa Khamis.
Aidha katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohamed Haji, alitaka kujua mpango wa Serikali wa utoaji elimu kwenye mifumo inayoanzishwa.
Mhe Chande alisema kuwa Serikali kupitia Taasisi zake imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu siku hadi siku kwa wadau wake kulingana na uhitaji katika kipindi hicho.