Na Fauzia Mussa. Maelezo.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amewahimiza akina mama wajawazito kuhudhuria Kliniki mapema ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao kazi cha kujadili kuendeleza mpango wa kumlinda mama na mtoto (M-MAMA Zanzibar) katika Hotel ya Ocean View Kilimani Mjini Unguja.
Amesema kuwa vifo vingi vinavyotokezea vya mama na mtoto vinatokana na baadhi ya akina mama kutohudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito na kujifungua nyumbani jambo ambalo linapelekea madhara mbalimbali ikiwemo kifo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikosi kazi cha mpango wa M-MAMA Zanzibar Mohammed Habib amesema lengo la mpango huo ni kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua Zanzibar.
Nae Msimamizi wa mpango wa M-MAMA Kitaifa kutoka Vodafone amesema ni wajibu wa kila mwanafamilia kuhakikisha anautumia mpango huo na kumuwahisha hospitali mama na mtoto ili kuokoa Maisha yao.
Kikao kazi cha kujadili mpango wa M-MAMA kiliwashirikisha wataalamu na wadau mbalimbali wa mama na mtoto.