……………..
Mwenyekiti wa Bodi ya Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt.Oswald Masebo amesema Serikali imeweka thamani kwa Makumbusho ya Taifa la Tanzania kama Taasisi muhimu ya kimkakati kwa ustawi wa Taifa kwa kuridhia marekebisho ya muundo na sheria ya Taasisi hiyo.
Dkt.Masebo ametoa kauli hiyo leo tarehe 25 Aprili 2024 wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa kilichofanyika katika kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam.
“Ushahidi wa thamani hii upo katika mambo ya kisera na kimkakati yaliyofanywa na Serikali amesema Dkt. Masebo na kuongeza kuwa kusainiwa kwa Sheria ya Mambo ya kale na kupitishwa kwa muundo mpya wa Taasisi unawezesha Makumbusho na Malikale kurejesha hadhi yake kama nguzo muhimu ya Taifa.
“Bodi inatambua kwamba haya ni matokeo ya kazi nzuri mnayoifanya ninyi watumishi wa Shirika, ninawaasa ongezeni bidii katika kazi” amesisitiza Dkt.Masebo
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt.Noel Lwoga ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Makumbusho ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuhifadhi urithi wa asili na utamaduni wa Tanzania na kubainisha Mpango Mkakati wa Mabadiliko ya kimuundo ndani ya Shirika hilo itakayowezesha kuwepo kwa mifumo mizuri ya kuzalisha mapato na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo ya Makumbusho na Malikale.
“Ni dhahiri haya yote yanaonesha kuwa Makumbusho inabadilika, na hii inaendana na falsafa ya Mhe. Rais Samia ya ‘Reforms’, Makumbusho inakwenda kuzaliwa upya, tuko katika enzi mpya na mweleko mpya, na Makumbusho mpya, haya mazuri yote yaliyofanywa na wafanyakazi tumepata fursa ya kuwapa hamasa ili kuboresha zaidi utendaji kazi’’ amesema Dkt.Lwoga
Wakizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wengine Afisa Rasilimali watu kutoka Makumbusho ya Taifa Bw.Morris Pemba na Mhifadhi kutoka Kijiji cha Makumbusho, Bi. Flora Vicent wamesema uwepo wa vikao vya Baraza la Wafanyakazi unawawezesha kukumbuka majukumu yao, kuelewa mwelekeo wa taasisi, kufahamu mafanikio kujadili njia bora zaidi za kukabiliana na changamoto mbalimbali.