Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kuwa ina lengo la kuboresha maisha ya wananchi wa tarafa hiyo kwa kuwaelimisha na kuwahamisha wananchi waliojiandikisha kuhama kwa hiyari kwenda Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga na maeneo mengine nchini.
Akizungumza na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwa nyakati tofauti katika zoezi la uelimishaji, uhamaishaji na uandikishaji kaimu meneja wa Uhusiano kwa Umma wa mamlaka hiyo Hamis Dambaya amesema zoezi la kuwaelimisha wananchi hao litaendelea ili kuhakikisha kila mkazi wa tarafa ya Ngorongoro anahama kwa hiyari.
Amewaeleza wananchi hao kwamba serikali haina nia mbaya kwa kuwashawishi kuhama kutoka ndani ya hifadhi kwani inatambua kuwa iwapo wananchi hao watakubali kuhama wataweza kuboresha maisha yao katika maeneo mbalimbali watakayoamua kuelekea sambamba na kulinda usalama wao kutokana na uwepo wa matukio ya wanyama wakali ndani ya hifadhi.
“Mnaishi katika mazingira magumu hasa kutokana na kukosa uhuru wa kuingia na kutoka ndani ya hifadhi, kuhofia Wanyama wakali ambao wamekuwa hatari kwa mifugo na baadhi ya wananchi, serikali imefanya uamuzi sahihi wa kuwahamasisha ili kuwa na Maisha bora na huru nje ya hifadhi,”alisema bwana Dambaya.
Bwana Dambaya amesisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha kila mwananchi anayekubali kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi anapata stahiki zake zote za kisheria ikiwemo kitita cha shilingi milioni kumi wanaohamia msomera na shilingi Milioni kumi na tano wanaohamia maeneo mengine ambapo fedha hizi zinatolewa kama motisha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amewataka wananchi hao kuachana na propaganda za baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wasiowatakia mema kwa kuwashawishi kuendelea kubaki ndani ya hifadhi huku wao na familia zao wakiishi katika miji mbalimbali nchini na kufanya shughuli zao katika mazingira magumu.
“Msihadaike na watu wenye nia ovu wanaowashawishi mbaki ndani ya hifadhi, hameni kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine ambayo huduma za kijamii zimeboreshwa kwa mustakabali wenu na vizazi vyenu”,alisema bwana Dambaya.
Katika ziara hiyo ya tarafa ya Ngorongoro timu ya uhamasishaji imeweza kutembelea kaya mbalimbali katika Kijiji cha Naiyobi, Kapenjiro na endulen ambapo wananchi kadhaa walielimishwa na kukubali kuhama kwa hiyari na kuamua kujiandikisha.