Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala amewaongoza mamia ya wakazi wa eneo hilo kwenye mkesha wa maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Lulandala akizungumza kwenye mkesha huo ambao umetumika pia kumsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumza mbashara na watanzania kwa njia ya runinga amesema wana Simanjiro wameitikia vyema tukio hilo.
Hata hivyo, DC Lulandala amekabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi mbalimbali ikiwemo wa mpira wa miguu na mashindano ya insha.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya (DED) Simanjiro, Dominica Ngaleka amesema kulifanyika tamasha la michezo na mashindano ya insha kwa wanafunzi.
“Timu ya veterani wamekuwa mabingwa wa mpira wa miguu na kwa upande wa insha mshindi wa kwanza John Mollel ametoka shule ya sekondari Simanjiro na mshindi wa pili amechukua mwanafunzi wa shule ya msingi Mapinduzi Samwel Mkude,” amesema Ngaleka.
Katibu Tawala DAS wa Wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid Maulid amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kumsikiliza mbashara Rais Samia kupitia runinga.
“Nawashukuru kwa kujitokeza kwa wingi na pia kumsikiliza Rais Samia kwenye hotuba yake ambapo amewasisitiza watanzania kudumisha muungano,” amesema DAS Warda.
Diwani wa kata ya Orkesumet Sendeu Laizer amewapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kujitokeza kwa wingi kwenye kushiriki mkesha huo wa maadhimisho ya miaka 60 ya muungano.
“Wananchi wa Orkesumet mmefanya vyema kwenye mahudhurio kwani mmejitokeza kwa wingi kwenye mkesha na pia mmesikiliza Rais Samia kupitia runinga mbashara,” amesema Sendeu.