Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke, Ismail Bukuku akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2024.
Afisa Mawasilinao wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke Neema Kilongozi akiwa katika mkutano na waandishi wa habari.
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Ismail Bukuku uliofanyika leo Aprili 24, 2024 katika Ofisi za takukuru mkoa wa temeke zilizopo Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam.
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imefatilia utekelezaji miradi miwili yenye thamani ya shillingi milioni 700,000,000 inayotekelezwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni na kubaini uzembe uliofanywa na baadhi ya watumishi na kusababisha kuchelewesha uanzishaji wa miradi kinyume na maelekezo ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI).
Miradi hiyo ni ujenzi wa Shule mpya mbili za Sekondari ya Vumilia Ukooni na Mbutu zenye thamani ya shilingi milioni 350,000,000 kwa kila shule.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 24, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2024, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Temeke, Ismail Bukuku, amesema kuwa baada kufatilia na kuwasilisha matokeo ya ufuatiliaji kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo watumishi waliohusika na uzembe huo walichukuliwa hatua za kinidhamu.
Bukuku amesema kuwa Watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu ni aliyekuwa Mkuu wa Divisheni Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Kigamboni Bi. Restituta Mtaita pamoja na aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi Manispaa ya Kigamboni Bw. Joseph Mhere.
“Natoa wito kwa watumishi wote kutimiza wajibu wao wa kusimamia kwa uadilifu na uaminifu miradi yote kwa kuwa wameaminiwa katika taasisi wanazohudumia, kwa kuwa kutofanya hivyo ni kinyume na kifungu 31 cha PCCA“ amesema Bukuku.
Bukuku amefafanua pia wamefanikiwa kudhibiti ujenzi wa maghala matatu (godowns) katika eneo la Buza Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam kutokana uliokuwa unafanyika tofauti na kibali cha ujenzi kilichotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke.
“Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke alitoa kibali cha ujenzi wa ghala moja, kutokana na hali hiyo kanisa lilitozwa faini ya kiasi cha shillingi milioni 14, 134, 439.30“ amesema Bukuku.
Amesema kuwa wamepokea malalamiko 54 yanayohusu rushwa na kufanyiwa uchunguzi ili kuthibitisha tuhuma na zipo katika hatua mbalimbali, huku akieleza kuwa wamefanikiwa kufungua kesi moja na 16 zinaendelea Mahakamani.
Bukuku amesema kuwa wanatarajia kuendelea kuimarisha juhudi za kuzuia rushwa kwa kuongeza ushiriki kwa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la rushwa kwa kutoa huduma za jamii, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha ushiriki katika vita dhidi ya rushwa kupitia programu mbalimbali ikiwemo TAKUKURU Rafiki.
Ameeleza kuwa wamefanya kazi za kuimarisha klabu za wapinga rushwa kwenye shule za sekondari, msingi na vyuo 41 pamoja na kufanya mikutano ya hadhara 45, kutoa semina 17 kwenye idara mbalimbali na kutoa elimu kupitia vyombo vya habari.
”Wananchi wote wanapaswa kushiriki katika kusimamia miradi ya umma na kutoa taarifa mapema TAKUKURU kuhusu miradi inayotekelezwa katika maeneo yao pale wanapoona miradi imekwama au kuna ubadhilifu wa aina yoyote umefanyika“ amesema Bukuku.