Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge Viti Maalum aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa Taasisi za Fedha zinatoa mikopo yenye riba kubwa kinyume na muongozo wa BoT.
…………………..,
Na. Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera, kiutawala na kisheria ili kudhibiti tabia ya baadhi ya taasisi za fedha kutoa mikopo kinyume na miongozo iliyopo.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge Viti Maalum aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa Taasisi za Fedha zinatoa mikopo yenye riba kubwa kinyume na muongozo wa BoT.
Mhe Chande, alisema kuwa Serikali imekuwa ikiendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Fedha inayolenga kusimamia ukwasi katika mfumo wa kibenki ili kuendana na mahitaji halisi ya kiuchumi na kuweka mazingira rafiki ya utoaji mikopo.
“Serikali imekuwa ikiendelea kuhimiza benki kuwasilisha taarifa za wakopaji pamoja na kutumia kanzidata ya taarifa za wakopaji (credit reference bureau) wakati wa uchambuzi wa maombi ya mikopo ili kupunguza vihatarishi vya ongezeko la mikopo chechefu”, alisema Mhe. Chande.
Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fedha ili kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu fursa za mikopo zilizopo, viwango vya riba na athari zake, vigezo vya kuzingatia pamoja na umuhimu wa kurejesha mikopo.
Aidha Mhe. Chande alisema Serikali imekua ikiitisha vikao mbalimbali vya majadiliano na wadau katika sekta ya fedha ili kutambua changamoto zilizopo na kushirikishana mikakati ya kukabiliana nayo.
Alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya kaguzi, ufuatiliaji na tathmini ya uzingatiaji wa sera, sheria na miongozo iliyopo ili kuboresha na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wanaobainika kukiuka taratibu.
Katika swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti maalam Mhe.
Shally Josepha Raymond, aliyetaka kufahamu hatua zitakazochukuliwa na Serikali kwenye Makampuni ya Simu nchini yanayoendelea kutoa mikopo inayojulikana kama kausha damu bila wananchi kujaza fomu.
Aidha Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson amemuelekeza Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kufuatilia suala hilo na kulipatia taarifa sahihi.