NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Katibu wa Chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini Issack Kalleiya amekemea vikali tabia ya baadhi ya wanachama kuanza kufanya kampeni za chini chini na kutangaza nia kwa ajili ya kuwania nafasi mbali mbali za uongozi kabla ya muda kitu ambacho ni kinyume kabisa na taratibu za chama.
Katibu huyo ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi kata ya kongowe yenye lengo la kuweza kuzungumza na wanachama wa CCM ikiwa pamoja na kuimarisha uhai wa chama kuanzia ngazi za matawi,mashina pamoja na Kata husika.
Kalleiya ambaye katika ziara yake aliambatana na viongozi mbali mbali wa chama alisema kuwa lengo kubwa ni kuweka misingi imara ya kukijenga chama kuanzia katika ngazi za chini hadi ngazi za juu.
Aliongeza kuwa anashangazwa kuona baadhi ya wanachama kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa kwa kuanza kutangaza nia kinyemela ya kuwania katika nafasi mbali mbali za uongozi.
“Nipo katika ziara yangu yemye lengo la kuona namna ya kusimamia mwenendo mzima kwa wanachama ili waweze kuimarisha uhai mzuri kuanzia katika ngazi za matawi,mashina na ngazi nyingine,”
“Kitu kingine ambacho nakemea vikali ni hili suala la baadhi ya wanachama kuanza kufanya kampeni za chini chini za kutaka kuwania nafasi mbali mbali za chama kwa kweli hii sio sahii kwani muda wake ni bado,”alisisitiza Katibu Kalleiya.
Aliongeza katika chama cha mapinduzi kuna miongozo ambayo ipo wazi katika mambo ya uchaguzi hivyo ni lazima kila mwanachama anapaswa kuwaacha viongozi waliopo madarakani wamalize muda wao bila kuvunjiwa heshima.
Katibu huyo pia alliwahimiza wanachama wote wa ccm kuhakikisha kwamba wanajisajili kwa mfumo mpya wa njia ua kieletroniki ili waweze kutambulika kwa urahisi.
Alisema kwamba kwa sasa chama kinaendelea kuwahimiza wanachama wake kufanya uchaguzi mbali mbali ili kuweza kujaza nafasi nafasi ambazo bado zimeachwa wazi.
Katika aliongeza kuwa chama cha mapinduzi kikiimarisha kuanzia katika ngazi za chini kitaweza kuleta matokeo chanya na kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa serikali za
mitaa ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025.