Arusha, 23 Aprili 2024. Exim Bank, kupitia Mpango wake wa Kuwawezesha Kiuchumi Wanawake (WEP), imetoa mafunzo kuhusu masuala ya ujasiriamali, biashara, na uwezeshaji kwa wanawake wajasiriamali kama sehemu ya kuunga mkono ujumuishwaji wa watu wote, wakiwemo wanawake, katika mipango mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Kupitia mpango wake wa ‘Exim Cares’, mwaka jana (2023) Exim Bank ilizindua Mpango wa Kuwakwamua Kiuchumi Wanawake ujulikanao ‘Women Empowerment Program (WEP)‘ wenye lengo la kuongeza ushirikishwaji na kuleta usawa kwa wanawake barani Afrika, hasa katika nchi ambazo zina matawi ya benki hiyo ikiwemo Tanzania, Comoros, Djibouti na Uganda.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Exim Bank, Stanley Kafu, anasema, “Ukiwa mwaka wa pili mfululizo wa mpango wa Kuwakwamua Wanawake Kiuchumi (WEP), Exim Bank tunafuraha kubwa kuwa sehemu ya mafanikio haya na tunawapongeza washiriki wote kwa kuanza na kumaliza salama mafunzo haya kuhusu ujasiriamali, uwezeshaji, na biashara.”
Washindi watatu, wa awamu hii ya kwanza mwaka huu, walipata zawadi za pesa taslimu zilitolewa kwa washindi watatu ambapo mshindi wa kwanza, Beatrice A. Msafiri, akizawadiwa kiasi cha TZS 8,000,000, mshindi wa pili, Catherine Assenga akipata TZS 5,000,000 na mshindi wa tatu, Rukia S. Mohamed akiondoka na TZS 3,000,000. Pia, wahitimu wote walipata fursa ya kuweza kupata mikopo bila riba kutoka Exim Bank ili waweze kujiendeleza kiuchumi.
Exim Bank inaamini uwezeshaji wa wanawake na ujasiriamali unabaki kuwa sehemu muhimu ya mipango ya maendeleo nchini Tanzania na barani Afrika kijumla. Hii inadhihirishwa na ongezeko la idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi katika sekta mbalimbali kama siasa, kijamii na kiuchumi.
Akielezea kuhusu malengo ya mradi, Kafu alisema, “Mpango huu utakuwa ni endelevu kwa muda wa miaka mitano na tunatarajia kuwafikia wanawake zaidi ya 600,000 ifikapo mwaka 2028.”
Kafu anasisitiza kuwa Mpango wa WEP ni sehemu ya mkakati mkubwa na wa kina unaolenga kutengeneza jukwaa la wanawake ili waweze kufanikiwa na kustawi katika maisha yao, hasa kwenye eneo la uchumi.
Exim Bank imekuwa na itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote. Programu hii inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2025 na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050 na itakuwa chachu katika kuimarisha ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa wanawake.