Na.Elisa Shunda, Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Wazazi Tanzania Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Salum Hapi (MNEC) amempongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Kimataifa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kukamilika kwa asilimia kubwa.
Kauli hiyo aliitoa Jijini Dodoma jana, alipotembelea mradi huo na kuiona treni hiyo ya kisasa iliyokuja na viongozi mbalimbali wa dini, serikali na wafanyakazi wa Shirika la Reli *(TRC)* wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Ndg.Masanja Kadogosa, pamoja na waandishi wa habari.
Viongozi hao walikuja Dodoma kwa ajili ya kushiriki Dua Maalumu ya Kuliombea Taifa iliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Phillip Isdor Mpango.
Aidha Hapi, alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuwezesha majaribio ya treni hiyo kufanyika na mabehewa yake kuwasili nchini na kufanyiwa majaribio yanayotoa matokeo chanya.
Alisema amepata bahati ya kushuhudia ndoto za Watanzania na Rais Dk. Samia ameufikisha mradi huo katika kiwango kizuri.
“Nikiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, niliona ni vyema nije mwenyewe kuona, tunampongeza Rais kwa kazi kubwa, nzuri na ya kishujaa aliyoifanya katika mradi huu wa SGR na sisi tutaendelea kumsemea, kumuombea kwa Mungu na kumpongeza kwa uwekezaji mkubwa sh.trilioni 23.3,” alisema.
Hapi alisema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa kwa sababu uwekezaji alioufanya unahitaji dhamira, uongozi mzuri na udhubutu wa hali ya juu kwa sababu ni fedha nyingi alizowekeza.
“ Rais Dk.Samia amethibitisha kwa viwango vya juu kwamba ni mzalendo, ana mapenzi makubwa na nchi na amebeba maono ya taifa, kwa sababu mambo mengine inabidi uyabebe kama maono nchi yetu ifike wapi, usipokuwa na maono na kusema uingie na mambo mengine yatakayokuwa na matokeo ya muda mfupi matokeo yake taifa halitapiga hatua kubwa.
“Hivyo Rais Dk.Samia ameonesha anayo maono na ameyabeba maono haya ya kutupeleka katika nchi yenye treni ya kisasa,” alisema.
Hapi alisema ameridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Shirika la Reli Tanzania(TRC) kwa kuchukua ndoto za Rais Dk.Samia na kuzitekeleza.
“Sisi kama viongozi tuliofika kujionea hapa, tumeridhishwa na kazi nzuri mliyoifanya, tunapongeza utekelezaji wa Ilani ambao mmeufanya TRC na tunakupongeza wewe mwenyewe (Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa) kwa uongozi mzuri wa kuchukua maono na ndoto za Rais Dk.Samia kutufikisha hapa tulipo, tumeshuhudia Tanzania inakwenda,” alisema.
Hapi alisema lazima wamtetee Rais Dk. Samia,wamsemee na serikali ya CCM, haya mambo ili yatokee yanahitaji uongozi, ushupavu na uhodari mkubwa, hivyo hawawezi kumuacha peke yake.
“Hatuwezi kumuacha Rais Dk. Samia peke yake na wale wanaosema kwa nini tunamsifu Rais, tutaendelea kumsifu, kumpongeza na kumtia moyo kwenye mambo kama haya kwa sababu ni wajibu wetu kumtia moyo ili apate utulivu na ari ya kufanya mambo makubwa zaidi kwa taifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, alitoa shukurani kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi kutembelea mradi.
“Sisi watumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) hujisikia ufahari wa hali ya juu inapotokea nafasi ya viongozi wa CCM na Jumuiya zake wanapotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya mwendokasi na kusifia kwa kile kilichofanyika inatia moyo na morali wa kuendelea kutumikia shirika na serikali kwa maslahi mapana ya nchi,” alisema.
Hata hivyo, msafara wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Hapi, aliongozana na Naibu Katibu Mkuu Wazazi Bara, Joshua Chacha Mirumbe, viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, Wilaya na Kata husika kutembelea na kutazama mradi huo.