Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha ripoti ya hali ya Mazingira ya pwani na bahari ya Zanzibar huko Verde Mtoni Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Kapten Hamad Bakar Hamad akielezea kuhusiana na kitabu cha bahari ya Zanzibar katika uzinduzi wa kitabu hicho uliyofanyika Verde Mtoni Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya kale Mhe. Dk. Aboud Suleiman Jumbe akibadilishana mawazo na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha ripoti ya hali ya Mazingira ya pwani na bahari ya Zanzibar huko Verde Mtoni Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia uzinduzi wa kitabu cha ripoti ya hali ya Mazingira ya pwani na bahari ya Zanzibar huko Verde Mtoni Zanzibar.
PICHA NO.05:- Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhew. Othman Masoud Othman akimkabidhi kitabu cha ripoti ya hali ya Mazingira ya pwani na bahari ya Zanzibar makamu mkuu wa chuo kikuu cha Taifa SUZA Prof. Mohamed Makame Haji wakati wa uzinduzi wa vitabu hivyo uliofanyika Verde Mtoni Zanzibar. (PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR)
……….
Na Fauzia Mussa Maelezo
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman amewataka wataalamu walioandika kitabu cha ripoti ya hali ya mazingira ya pwani na bahari ya Zanzibar kuendelea kukusanya taarifa za elimu ya bahari kutoka kwa wenye uelewa ili kuandika zaidi taarifa zinazohusiana na mambo hayo.
Akizindua vitabu hivyo huko Verde Mtoni Zanzibar Mhe. Othman amesema vitabu hivyo vilivyotafitiwa na kuandikwa na wataalamu wazalendo vitaisaidia jamii na wageni wanaotembelea nchini kufahamu uhalisia wa mambo hayo.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na bahari na mazingira ya ukanda wa pwani yaliyo bora na ustahmilivu kwaajili ya maendeleo endelevu ya Visiwa vya Zanzibar hivyo kuipa umuhimu sekta hiyo kutapanua fursa za kiuchumi,kijamii,na kimazingira katika maeneo ya ukanda wa pwani na baharini na kuyafikia kwaharaka maendeleo endelevu ya 2030.
“kitabu hichi cha ripoti ya hali ya mazingira ya pwani na bahari yetu kutatoa tathmini sahihi ya kisayansi kuhusu mafanikio na changamoto za kuhifadhi na kusimamia mazingira.”
Amefahamisha kuwa sekta za utalii,usafiri wa baharini ,bandari,gesi asilia , mafuta pamoja na uvuvi zinachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa hivyo ipo haja ya kutambuliwa na kupewa kipaumbele.
Washiriki katika uzinduzi huo wamesema vitabu hivyo ni chachu ya mabadiliko na maendeleo ndani ya Zanzibar hasa katika sekta ya utalii na uchumi wa buluu.
Katika hafla hiyo Viongozi mbalimbali wa Serikali walishiriki wakiwemo Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Watendaji, Maafisa Wadhamini , Asasi za Kiraia pamoja na Wasomi na Wanataaluma.