Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Elizabeth Mokiwa akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2024.
…………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia utekelezaji miradi sita yenye thamani ya shillingi bilioni 61, 910, 746, 284.42 ikiwemo mradi wa ujenzi wa uwanja michezo Mwenge ambao umekamilika kwa asilimia 92.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi 2024, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Elizabeth Mokiwa, amesema kuwa mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo Mwenge wenye thamani ya shilingi bilioni 4,065, 100, 285.25 wanaendelea kufatilia ili kuhakikisha unakamilika kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha.
Mokiwa amesema kuwa mradi mwengine ni ujenzi wa mtandao wa maji taka na vituo viwili vya kusukuma maji wenye thamani ya shillingi 52, 407, 401, 646. 15 ambao umefika asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Novemba 24 kwa mujibu wa mkataba.
“Tumefatilia miradi yote na tumebaini mapungufu machache ambayo wahusika wameshauriwa kurekebisha, tunaendelea kufatilia kwa ukaribu hadi miradi itakapokamilka na kuhakikisha inakuwa bora kwa kuzingatia thamani ya fedha” amesema Mokiwa.
Mokiwa amefafanua kuwa wamepokea malalamiko yaliyohusu rushwa 40 ambapo yanaendelea kufanyiwa kazi ili kupatiwa ufumbuzi, huku akieleza kuwa mashauri mawili yametolewa maamuzi na Jamhuri imefanikiwa kushinda pamoja na kufungua mashauri mapya matatu na mashauri 19 yanaendelea Mahakamani.
Amesema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni inaendelea na mikakati ya kutoa huduma inayowafikia wananchi wote kupitia utekelezaji wa programu ya TAKUKURU – Rafiki ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwa kuwafikia wananchi pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo wenye jukumu la kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU na kuwasihi wanapopata taarifa zozote za Rushwa watoe taarifa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi kwa namba ya dharura 113- Bure” amesema Mokiwa.