Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 120, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Sima Constantine Sima (katikati) kwa ajili ya udhamini wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa utakaofanyika kuanzia leo jijini Zanzibar. Kushoto ni Afisa Mkuu Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao, Kulia ni Meneja wa Biashara wa Benki ya NMB Zanzibar, Naima Said Shaame (kulia) na Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT Taifa, Mohammed Maje (wa pili kulia). (Na Mpiga Picha Wetu).
……..,.,…..
BENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. Mil. 120 kudhamini Mkutano Mkuu wa 38 wa Mwaka wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT Taifa), unaofunguliwa Jumanne Aprili 23 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ukiwakutanisha washiriki zaidi ya 600.
Kiasi hicho kinachodhamini mkutano wa mwaka huu unaofanyika chini ya kaulimbiu; ‘Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Jambo Letu; Shiriki kwa Maendeleo ya Taifa,’ kinafanya udhamini wa NMB kwa ALAT Taifa kufikia Sh. Bil. 1.2 katika kipindi cha miaka nane.
Mkutano Mkuu wa ALAT, unaowapa fursa viongozi wa Serikali Kuu kutoa Maelekezo na Miongozo ya Kisera kwa Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wakiwemo Mameya wa Majiji na Manispaa, Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmshauri 184 (za Tanzania Bara), utafungwa Aprili 25 na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa miaka nane sasa, NMB na ALAT zimekuwa na ushirikiano endelevu katika masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Halmashauri zote nchini, ikiwemo kudhamini na kufanikisha vikao na Mikutano Mikuu ya Mwaka ya ALAT, ambayo kimsingi ndio chachu ya utendaji bora kwa Halmashauri hizo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, iliyofanyika Golden Tulip Zanzibar Airport Hotel, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema wanajivunia kuwa wabia wakubwa wa ALAT, na kwamba wanathamini heshima ya kipekee wanayopewa na uongozi wa jumuiya hiyo.
“NMB tunajivunia ubia baina ya benki yetu na Jumuiya hii, lakini pia tunathamini sana heshima ya kipekee ambayo tumekuwa tukipewa na Uongozi wa ALAT Taifa ya kujumuika pamoja nao katika Mkutano Mkuu huu muhimu kwa maendeleo ya Halmashauri zetu nchini.
“Kwa siku zote za Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa, tutakuwa na banda letu nje ya ukumbi wa mkutano, ili kuhakikisha wajumbe wa kikao pamoja na wadau wengine watakaokuwa katika maeneo ya Golden Tulip Hotel, wanapata huduma za kifedha wakati wote wa kikao.
“Nitumie nafasi hii pia kuwaalika wote katika banda la NMB kupata Huduma Jumuishi za Kifedha muwapo katika mkutano huo, na niwakikishie tu kwamba wafanyakazi wetu watakuwepo kutoa huduma na ushauri kwa wajumbe kwa wakati wote,” alisema Bi. Zaipuna.
Aidha, sambamba na udhamini huo, Bi. Zaipuna alibainisha kuwa, NMB imeandaa mchapalo kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa, ambako aliwakaribisha kushiriki chakula cha jioni, pamoja na kujadiliana machache baina ya Wajumbe ALAT na wafanyakazi wa NMB.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Bw. Sima Constantine Sima, aliishukuru NMB kwa ubia endelevu unaowawezesha kufanikisha vikao na Mikutano Mikuu ya kila mwaka kwa kipindi cha miaka nane sasa ya udhamini wao.
“Shukrani za Jumuiya yangu ziifikie Benki ya NMB kwa hiki inachofanya katika kufanikisha Mikutano Mikuu ya ALAT Taifa kwa miaka nane sasa na hii ndio tafsiri sahihi ya mahusiano mema na ya muda mrefu, ambayo sisi ALAT ndio wanufaika wakuu.
“NMB sio tu wadau wetu kibiashara, bali wao wamekuwa moja ya sehemu kuu za sisi kutolea huduma zetu. Mambo mengi yanayoendelea kufanyika katika Halmashauri zetu yanapitia kwao na ndio ushuhuda wa hili na mahusiano haya ndio tafsiri sahihi ya tunayoyaona kwa miaka nane ya udhamini wao.
Nichukue nafasi hii kuishukuru NMB kwa kutafsiri kwa vitendo juu ya mahusiano mema, ambapo leo pia imedhamini uzinduzi wa kimapinduzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Zanzibar (ZALGA), ambayo ni mamlaka sawa na ALAT kwa huku visiwani Zanzibar,” alisema Sima.
Aidha, aliishukuru NMB kwa kuandaa hafla ya chaklula cha usiku baina ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ALAT Taifa na Wafanyakazi wa NMB, na kwamba anaamini mchapalo huo utakuwa fursa nzuri sio tu ya kubadilishana Mawazo, bali kufurahi pamoja baada ya kazi.