Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akisisitiza jambo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala (hayupo pichani), kuhusu huduma
zinazotolewa TEMESA, jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala akisikiliza
kwa makini maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani),
alipohoji utoaji wa huduma za vivuko nchini.
Muonekano wa Kivuko cha MV Tanga ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 100,
magari 6 sawa na tani 50.
…………………….
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kuwasilisha majina ya Mameneja wa Kanda na
Mikoa wa TEMESA ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia
wananchi ili waweze kuchukuliwa hatua.
Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma kufuatia kupokea
malalamiko mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA ikwemo
huduma ya Kivuko cha MV.Tanga Mkoani Tanga ambapo amemuagiza Katibu Mkuu
kuingilia kati kubaini changamoto zinazokwamisha kivuko hicho.
“Mambo mengi ya kiutendaji yanaletwa kwa Waziri na Katibu Mkuu wakati Watendaji
mpo na tumewaamini kusimamia Taasisi zenu, hasa jambo hili lipo TEMESA. Mtendaji
Mkuu kama kuna mapungufu ya wasaidizi wako bora uje kwa Katibu Mkuu useme huyu
atufahi aondoke kuliko kukaa nao maana hatimaye litakuangukia wewe”, amesema
Bashungwa.
Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour
kuangalia namna bora ya usimamizi wa TEMESA katika huduma ya vivuko nchini ili
kuleta manufaa na uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ziimarike.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa bado TEMESA inaendelea kuwa na mikwamo na
kutotekeleza majukumu yake kwa uharaka pindi tatizo linapogundulika katika Vivuko na
hivyo kupelekea kuzorota kwa huduma hiyo katika baadhi ya maeneo.
“Changamoto ya marekebisho ya kivuko cha MV Tanga yanaendelea zaidi ya siku 10
sasa lakini leo naulizia vifaa bado havijafika, kama ‘parts’ ziko Dar es Salaam
inachukua masaa mangapi hadi kufika Tanga? na sio Tanga pekee yake ni maeneo
yenye vivuko”, Bashungwa akimuhoji Mtendaji Mkuu wa TEMESA.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala amekiri kuwepo kwa
changamoto hiyo katika Kivuko cha MV. Tanga na timu ya wataalam inaendelea na
marekebisho ya Kivuko hicho ili kuboresha huduma zake.