Na WAF – Dar Es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan atagharimia matibabu ya upasuaji na utengamao kwa watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yatakayofanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Aprili 21, 2024 alipotembelea Taasisi ya MOI kwa ajili ya kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa upasuaji chini ya ufadhili wa MO Dewji Foundation Jijini Dar Es Salaam.
Waziri Ummy amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa MOI Prof. Abel Makubi kuwasilianeni na ASBATH kujua watoto hawa 100 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji na huduma za utengamao kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Lakini pia, nimemsikia mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi wenye watoto wa tatizo hili la kichwa kikubwa na mgongo wazi kwamba wana watoto 200 wanaopaswa kufanyiwa upasuaji lakini wazazi hawana uwezo”. Amesema Waziri Ummy
Aidha, Waziri Ummy ameipongea Taasisi ya MOI kwa kutoa matibabu ya watoto hao na MO Dewji Foundation kwa ufadhili wa matibabu ya watoto 50, huku akiwataka wadau kuendelea kujitokeza kusaidia wengine.
“Kubwa nataka kutoa wito kwa wazazi wenzangu kwa wale wenye watoto wenye changamoto hii ya vichwa vikubwa na mgongo wazi wasiwafiche watoto hao, wahakikishe wanawapeleka kliniki ili wapate ushauri wa kitaalam”. Amesisitiza Waziri Ummy
Kwa upande wake daktari bingwa mbobezi wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu MOI, Dkt. Hamisi Shabani amesema tatizo la vichwa vikubwa linaweza kuzuilika kwa kuhakikisha wanaume wanawalisha wake zao vyakula vyenye madini ya Frolic Acid na kuwawahisha kliniki watoto wenye tatizo hilo.
Nae, Mkurugenzi wa MO Dewji Foundation Imran Sherali ameishukuru Serikali na taasisi ya MOI kwa kufanikisha matibabu hayo na kuongeza kuwa Taasisi hiyo ipo tayari kuendelea kupokea msaada kwa watoto wengine.