Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Vikundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wanachama wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) wakati akifungua mkutano mkuu wa 21 wa chama hicho uliofanyika leo Aprili 21, 2024 katika Hotel ya New Afrika, Dar es Salaam.
Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) Dkt. Zaituni Bokhary akizungumza jambo katika mkutano mkuu wa 21 wa chama hicho uliofanyika leo Aprili 21, 2024 katika Hotel ya New Afrika, Dar es Salaam.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Vikundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amekitaka Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kuongeza nguvu katika jitihada za kukabiliana na mila na desturi kandamizi katika jamii kwa ajili ya kuleta maendeleo stahimilivu kwa wanawake, wanaume pamoja na watoto.
Akizungumza leo Aprili 21, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa MEWATA uliofanyika katika hoteli ya New Afrika, Mhe. Dkt. Gwajima amesema kuwa wakati umefika kwa MEWATA kufanya kazi na wizara hiyo katika kuhakikisha wanatengeneza misingi imara ya watoto wa kike kwa kupata afya bora ili waweze kufanya vizuri na kuleta ushindani.
Dkt. Gwajima amesema kuwa ni vizuri kuweka mikakati ya kuendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuwawezesha wanawake kupata huduma za afya na kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“Ni muhimu kufanya kazi kwa ushirikiano katika utoaji wa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia kwa kuwezesha ujenzi wa vituo vya wanawake pamoja na vituo vya ushauri nasaha kwa walionusurika“ amesema Dkt. Gwajima.
Amebainisha kuwa mujibu wa Ofisi ya takwimu ya Utafiti wa Demografia na Afya 2015 – 2016 zinaonesha asilimia ya 40 ya wanawake wenye umri kati 15 – 49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili, huku asilimia 17 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.
“Jamii zetu bado zinakabiliwa na changamoto ya mila na desturi kandamizi ambazo zinazowazuia wanawake na watoto kufikia ndoto zao na kutoa mchango wao katika ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla“ amesema Dkt. Gwajima.
Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) Dkt. Zaituni Bokhary, amesema kuwa kuna changamoto nyingi zinawapata wanawake lazini wanashindwa kusema kutokana na mila potofu zilizopo kwa baadhi ya jamii.
Dkt. Bokhary amesema kuwa ili kufika malengo tarajiwa wamejipanga kutoa elimu kuhusu afya ya mwanamke katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vijijini.
“Tupo tayari kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuweka mipango rafiki katika kuhakikisha tunawafika walengwa na kuwapatia elimu hasa maeneo ya vijijini ambapo kunaonekana kuna uhitaji mkubwa” amesema Dkt. Bokhary.
Nae Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) Dkt. Marry Sando, amesema kuwa kupita taaluma zao kwa kushirikiana na wizara wataweza kutoa msaada na kutengeza jamii iliyokuwa na mstali mwema.
Amesema kuwa katika mkutano watapata fursa ya kujadili kwa namna gani wanaweza kutoa mchango wa kitaaluma katika afya ya mama na mtoto na jamii kwa ujumla.