Katibu Tawala wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Upendo Wella, amesema kwamba katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanikiwa kusimamia masuala ya Muungano kwa ufanisi mkubwa.
Hii imesababisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu, na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano.
Wella alitoa kauli hii wakati akiwaongoza wananchi katika zoezi la upandaji miti, ambalo ni sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Zoezi hilo lilifanyika leo katika Kata ya Kisima, wilayani Same.
Aidha,amewahimiza wananchi wa wilaya ya Same kuendeleza utamaduni wa kupanda miti katika sehemu mbalimbali, hasa kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha kwa wingi, ili miti iweze kustawi vyema na kuepukana na hali ya ukame.
Vilevile, amewaomba walimu wote kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda mti katika mazingira ya shule na kusimamia ukuaji na utunzaji wa mti huo, pamoja na kuhimiza upandaji miti majumbani, katika taasisi za serikali na zisizo za serikali, ili baadaye wilaya iwe na rutuba nzuri ya miti.
Katibu huyo pia amewaalika wananchi kushiriki katika mkesha wa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utakaofanyika tarehe 25, ambapo kutakuwa na matangazo ya moja kwa moja ya hotuba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia channel ya TBC.
Siku inayofuata, tarehe 26, ambayo ni Siku ya Muungano, wananchi watashiriki katika majadiliano ya masuala mbalimbali yanayoweza kujenga taifa.