Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameshiriki Mkutano wa 39 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji kuhusu uendelezaji wa viwanda vya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hususani katika kuendeleza viwanda vya nguo, ngozi, pamba, madawa, matunda na mbogamboga.
Mkutano huo unaofanyika jijini Arusha kuanzia Aprili 17-20, 2024 umehusisha Mawaziri wengine wa kisekta kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Mawaziri wengine kutoka Tanzania walioshiriki mkutano huo ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutoka Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe.