Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza na
wananchi wa mkoa huo waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni –
Kigoma kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa
zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo. Kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma Dkt. Jesca Leba.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Kawajika Mwinyipembe akimweleza Katibu Tawala wa mkoa wa
Kigoma Hassan Rugwa jinsi kipimo cha kuangalia moyo unavyofanya kazi
kinavyofanyika wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyofanywa na
wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Maweni – Kigoma.
Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa akizungumza na
madaktari wa watoto wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma na wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea hivi karibuni kambi ya
uchunguzi na matibabu ya moyo. Kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt.
Jesca Leba.
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Shamira Rwegoshora akimuelekeza jinsi mishipa ya
damu ya moyo inavyoziba kutokana na kuzidi kwa mafuta mwananchi aliyefika
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma kwaajili ya kupata huduma za
upimaji na matibabu ya moyo.
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwahudumia
wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma kwaajili
ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya
matibabu iliyomalizika hivi karibuni. Watu 351 walihudumiwa katika kambi hiyo
watoto wakiwa 65 na watu wazima 286 waliokutwa na matatizo yaliyohitaji
matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI ni 19 watoto
nane na watu wazima 11.
Afisa Lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma
Franciscka Lutumura akitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi waliofika katika
hospitali hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo
zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa hospitali hiyo kwa kushirikiana nawenzao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Watu 351 walihudumiwa katika
kambi hiyo watoto wakiwa 65 na watu wazima 286 waliokutwa na matatizo
yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI ni 19
watoto nane na watu wazima 11.
Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ireen Mbonde
akimkabidhi Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa vipeperushi vitoa
elimu ya kujiepusha na magonjwa ya moyo pamoja na huduma zinazotolewa na
taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo
iliyomalizika hivi karibuni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma.
……………..
20/4/2024 Serikali mkoani Kigoma imejipanga kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wanaendelea kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo kwa kuboresha huduma za matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma pamoja na kufanya kambi za matibabu ya kibingwa.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa wakati akizungumza na wananchi wa mkoa huo waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali hiyo.
Rugwa alisema Serikali imewasomesha wataalamu wa afya wa kutosha katika kada mbalimbali, imejenga hospitali na vituo vya afya vya kutosha pamoja na kununua vifaa vya kisasa vya kutibu magonjwa mbalimbali ndiyo maana huduma za kibingwa zinapatikana hapa nchini tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Wataalamu kutoka JKCI wameletwa na serikali kuja kutoa huduma, kutokana na uhitaji mkubwa uliopo tumeona siku walizokuja ni chache tumeichukuwa hii kama changamoto tunajipanga ili warudi tena hapo baadaye na kuwa na siku nyingi zaidi za kutoa huduma kwa wananchi”, alisema Rugwa.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eva Wakuganda alisema katika kambi hiyo wameona watu 351 kati ya hao watu wazima walikuwa 286 na watoto 65, watu 19 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Dkt. Eva alisema kwa upande wa wagonjwa waliopewa rufaa ambao watu wazima walikuwa 11 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwa ni pamoja na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo, kutanuka kwa moyo, shida za valvu na mfumo wa umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri.
“Watoto tuliowaona walikuwa 65 kati ya hao 45 tuliwakuta na matatizo mbalimbali ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu kutokukaa katika mpangilio wake. Watoto nane tumewapa rufaa ya haraka ili waje kutibiwa wiki ijayo katika taasisi yetu kwani tuna kambi kubwa ya upasuaji wa moyo kwa watoto”, alisema Dkt. Eva.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Maweni – Kigoma Dkt. Lameck Mdengo alisema licha ya wananchi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo lakini pia imewajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo ambao wamejifunza namna ya kuwatibu na kuwatambua wagonjwa wa moyo.
“Ninawashukuru sana wataalamu wenzetu wa JKCI ambao tumekuwa nao kwa muda wa siku tatu katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi, tumejenga uhusiano mzuri ambao utatusaidia kuwatibu wagonjwa wa moyo”.
“Katika Hospitali yetu tuna kliniki ya magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu mara mbili kwa wiki, wagonjwa wote ambao tumewakuta na shida katika kambi hii wataendelea kupata huduma za matibabu katika kliniki zetu. Tuna dawa za kutosha ambazo tumewapa wakazitumie ninaamini zitawasaidia katika matibabu yao”, alisema Dkt.Mdengo.
Nao wananchi waliopata huduma za matibabu katika kambi hiyo waliishukuru Serikali na kusema kuwa hii ni mara ya kwanza wataalamu wa magonjwa ya moyo wamefika katika hospitali hiyo kwaajili ya kufanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo na kuomba huduma hiyo ifanyike tena ili wananchi wengi zaidi hasa walioko vijijini wafaidike nayo.
“Nimefika hapa nimepima vipimo vyote vya moyo na kukutwa ninashida ya shinikizo la juu la damu, nimepewa dawa za kutumia ninaamini baada ya kutumia dawa hizi nitakuwa sawa”, alisema Ali Tambwe mkazi wa Kigoma Ujiji.
“Nilisikia ujio wa wataalamu hawa kupitia redio nami nikahamasika kuja kupima afya yangu nimefanyiwa vipimo vyote vya moyo niko sawa sina tatizo. Ninawasihi wananchi wenzangu zinapotokea nafasi kama hizi wajitokeze kwa wingi kuja kupima na kupata ushauri wa kitaalamu ukiwemo wa lishe ambao mimi nimeupata “, alisema Mederina mkazi wa Lake Tanganyika.