Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fatma Kabole akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiana na zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana kati ya umri wa miaka 9-14, inayotarajiwa kuanza April 22-25 nchi mzima, hafla ambayo imefanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Unguja.
……………..
Wizara ya Afya Zanzibar inatarajia kuendesha zoezi la chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 9 -14 ili kuwalinda na ugonjwa huo.
Akizungumza na Waandishi wa habari huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Wilaya ya Mjini, Naibu Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fatma Kabole amesema zoezi hilo linatarajia kuwafikia watoto zaidi ya laki moja katika Skuli za Serikali na binafsi.
Aidha amefahamisha kuwa kumewekwa utaratibu maalum wa kuwafikia watoto walioko majumbani kupitia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii ili kuweza kupata chanjo hiyo.
Amesema taakwimu zinaonesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kuathiri wananwake ambapo kiasi ya wananwake 466,000 wanagundulika na tatizo hilo kila mwaka wengi wao wanatoka nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.
Hivyo amewaomba Waalimu kusimamia chanjo hiyo sambamba na Wazazi na walezi kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake mratibu wa chanjo kitengo shirikishi afya ya uzazi na mtoto Abdulhamid Ameir Swaleh amewataka wazazi na walezi kupuuza taarifa potofu zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa chanjo hiyo inamadhara.
Aidha amesema chanjo hiyo ni salama kwani imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) kutumika kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 14.
Zoezi la utoaji wa chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi litazinduliwa rasmi tarehe April 22 katia skuli ya Abeid Karume Micheweni Pemba na kuendelea hadi April 25 katika Skuli za Serikali, binafsi na jamii.