…………………..
Na WMJJWM- Dar Es Salaam
Wanawake nchini wameendelea kupata fursa za uongozi katika ngazi mbalimbali huku takwimu zikionesha ongezeko la Wanawake katika uongozi ikiwemo Mawaziri Wanawake kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2005 hadi asilimia 37 kwa mwaka 2023. Aidha, Wabunge wanawake wameongezeka kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 37 kwa mwaka 2023.
Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa mradi wa “Think Equal Lead Smart” wenye lengo la kuhamasisha wanawake na vijana kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi uliofanyika jijini Dar Es Salaam Aprili 18, 2023.
Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema
takwimu zinaonesha pia Wanawake Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameongezeka kwa asilimia 38, Madiwani asilimia 29.9. Mabalozi asilimia 25, Makatibu Wakuu asilimia 22, Manaibu Makatibu Wakuu asilimia 28, Wakuu wa Mikoa asilimia 31, Makatibu Tawala asilimia 26, Wakuu wa Wilaya asilimia 33 na Wakurugenzi asilimia 28.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema Tanzania imeendelea kutambua umuhimu wa Wanawake kwa kuwapatia fursa katika nafasi za Uongozi na Maamuzi na kuongeza ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za Uwakilishi, Uongozi na ngazi za maamuzi. Mabadiliko haya yanatokana na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha kuna usawa kati ya Wanaume na Wanawake na katika nyanja zote.
Ameongeza kuwa Wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya familia na Taifa kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la watu nchini ni Wanawake ingawa bado wanawake wanakabiliwa na changamoto zinazowaathiri na kukwamisha maendeleo yao; miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uwepo wa mila na destruri zenye madhara, kutopatiwa fursa ya kupata elimu pamoja na kutoshirikishwa katika shughuli za ujasiriamali na uzalishaji mali.
“Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Kikanda na Kimataifa inayolenga kukuza Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake hapa nchini. Mikataba hiyo imekuwa chachu kwa maendeleo ya Wanawake ambapo kupitia Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, nchi yetu inatekeleza afua mbalimbali zinazochochea Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi.” amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha, Naibu Waziri Mwanaidi amesema Serikali inatambua mchango wa Mradi huo unaolenga kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika ngazi zote za maamuzi nchini Tanzania na ameahidi kuendelea kushirikiana Taasisi hiyo kuwafikia Wanawake hasa walio maneno ya pembezoni mwa nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CEO Roundtable of Tanzania Santina Benson amesema Taasisi hiyo imeanzisha mradi huo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha Wanawake wanaoata fursa sawa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi katika ngazi za maamuzi na fursa za kiuchumi.
“Mradi wa Think Equal Lead Smart (TELS) unaosimamiwa na Taasisi yetu unalenga kuwezesha ushiriki wa wanawake na fursa sawa za uongozi katika ngazi zote za maamuzi nchini Tanzania. Hivyo tunaomba Ushirikiano kutoka kwa Serikali na Taasisi nyingine ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu kwa pamoja” ameeleza Santina .