Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kujikita kwenye utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa kuwa mandhari yanayoonekana mkoani humo kwa sasa yanatokana na miti iliyopandwa na Wazee wetu miaka mingi iliyopita
Makonda amezungumza hayo mapema leo, Ijumaa Aprili 19.2024 wakati akiongoza zoezi la upandaji miti lililofanyika kwenye viunga vya Chuo cha Ualimu patandi, kilichopo wilayani Arumeru ambapo pamoja na mambo mengine amesema suala la upandaji miti na utunzaji wa mazingira ni sehemu ya maelekezo ya viongozi wa kitaifa akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango aliyemtaka kuhakikisha anasimamia kikamilifu jambo hilo
Amesema haikubaliki kuona mpaka sasa wakazi wa mkoa huo wanaendelea kujivunia miti iliyopandwa miaka mingi iliyopita wakati wanayo fursa ya kuweka mikakati thabiti ili ikiwezekana kila mwananchi ndani ya mkoa huo awe na mti wake, kwani kukosekana kwa miti kumękuwa kukisababisha athari za kimazingira ikiwemo mmomonyoko wa udongo
Ili kuhakikisha mpango unakuwa kabambe na unatekelezeka ipasavyo Mkuu wa mkoa huyo amesema atahakikisha anaandaa hafla maalum ya zoezi la upandaji miti kimkoa ambapo anaweza kumualika Makamu wa Rais Dkt. Mpango endapo ratiba itamruhusu ili aungane nao kwa pamoja
Akizungumzia suala la usafi Makonda ameeleza masikitiko yake kutokana na kukithiri kwa uchafu hususani kwenye jiji la Arusha hivyo kutoa maelekezo mahsusi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali mkoani humo wakiwemo Wakuu wa wilaya, na wananchi wote kwa ujumla, kila mmoja kwa nafasi yake kujitathimini na kuhakikisha anatekeleza usafi kuanzia kwenye mazingira yake yanayomzunguka na maeneo ya umma
Ameeleza masikitiko yake kufuatia ziara aliyoifanya hivi karibuni kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeidi, jijini Arusha alipoenda kukagua maandalizi ya kilele cha siku ya wafanyakazi Duniani inayotarajiwa kufanyika mkoani humo kitaifa Mei 01.2024 ambapo baadhi ya maeneo kukithiri uchafu ambao kwenye mazingira ya kawaida ni jambo lisilovumilika
Katika kuhakikisha jiji la Arusha linakuwa safi amesema anakusudia kuanzisha mazungumzo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kampuni yao ihusike kusimamia usafi jijini humo kwa kuwa kampuni hiyo amewahi kufanyanao kazi alipokuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na kwa kiasi kikubwa walifanikisha jambo hilo
Katika hatua nyingine Makonda ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Arusha kuhakikisha wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anafanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi, kwa kwa mkoa huo pekee pamoja na miradi mingine lakini amewapatia zaidi ya milioni 280 kwa ajili ya kufanikisha mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo utakaotimika kwa ajili ya michuano ya AFCON 2027
Aidha, ameendelea kusisitiza kuwa mkoa huo ni kinara kwenye masuala ya utalii Tanzania Bara hivyo wakazi wake hawana budi kujiweka tayari na kuchangamkia fursa zilizopo