*Waziri Mavunde akutana na Kampuni ya Perseus Dodoma leo
*Awataka kuharakisha uendelezaji wa mradi
*Asisitiza ukamilishwaji wa malipo ya fidia na uhamishwaji wananchi
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde leo amefanya kikao cha pamoja na Kampuni ya Perseus ya Australia ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wake Ndg. Jaffer Quartamaine juu ya uendelezwaji wa mradi wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ore Corp ambayo hisa zake zimenunuliwa na Kampuni ya Perseus.
Katika Mkutano huo Waziri Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa kufanikiwa kukamilisha wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuitaka Kampuni hiyo kukamilisha kwa uharaka malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha mradi.
Pia Waziri Mavunde amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaanza mapema uendelezaji wa mradi kwa mujibu ya makubaliano ya awali ya kimkataba ili nchi ianze kunufaika na matunda ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa dhahabu katika Wilaya ya Sengerema,Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza katika kikao hicho,Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Perseus Bw. Jaffer Quartamaine ameishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuahidi kwamba wamejipanga kuanza uendelezaji wa mradi huu mapema kadri iwezekanavyo kutokana na mpangilio wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi.
Ameongeza pia kwamba wamejipanga kufanya uwekezaji mkubwa na wa mfano kwa kutumia Teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu nchini.