Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya (kulia), akizungumza na waandishi wa habari,Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Nyamagana ilipotembea miradi ya Mfumo rahisi wa Uondoshaji na kuchakata majitaka katika Gereza Kuu la Butimba, leo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga wa pili kutoka kushoto,leo akizungumza na watumishi wa MWAUWASA wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Neli Msuya (wa pili kutoka kulia), a kwanza ni Meneja miradCelestine Mahubi,baada ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya kukagua mradi wa majitaka Butimba.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega (kushoto) akizungumza baada ya Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo kukagua mradi wa majitaka Butimba na baadaye mradi wa Matokeo ya Haraka Luchelele.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Nyamagna wakiangalia mradi wa mfumo rahisi wa uondoshaji na tiba ya majitaka katika Gereza Kuu la Butimba, leo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama wa wilaya, Peter Bega (wa pili kushoto),wa kwanza ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya.
………………….
Pongezi hizo zimetolewa na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nyamagana,leo ilipotembelea na kukagua miradi iliyotekelezwa mamkala hiyo.
Akitoa pongezi hizo, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga amesema kwa kipindi kifupi MWAUWASA chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Neli Msuya imefanya mambo makubwa ya kuhakikisha wananchi wa Jiji la Mwanza, wanapata maji safi na salama kwa matumizi ya kibinadamu.
Amesema utekelezaji wa mradi wa kuondosha na kutibu majitaka utaboresha usafi na mazingira na kuimarisha afya za wafungwa na watumishi wa Gereza Kuu la Butimba ikiwemo kuboresha maji ya Ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikuu cha maji jijini Mwanza.
“Kazi kubwa na nzuri umeifanya muda mfupi tangu ukabidhiwe kuisimamia MWAUWASA na tunakupongeza kwa ubunifu na utekelezaji ilani ya CCM kwa vitendo kwa maslahi ya wananchi.Mradi huu utaboresha mazingira na gereza la Butimba litapata huduma nzuri kwa wafungwa na watumishi,”amesema Kavenga.
Amewataka wanufaika kutunza miundombinu ya mradi itumike muda mrefu kwa sababu Nyamagana imependelewa kwa miradi ya kimkakati inayoonekana kwa macho na thamani yake ambapo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo kuboresha mazingira na maji.
Diwani wa Butimba (CCM),Marwa Mbusiro amesema mazingira ya Gereza la Butimba hayakuwa rafiki kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya vyoo,hivyo mradi huo utabadilisha mazingira na madhari ya gereza na kuleta tija kwa jamii ya wafungwa.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Butimba,Faustine Ntonja amesema gereza hilo lilikuwa kero kwa kutirisha maji sababu ya uchakavu wa miundombinu iliyojengwa kwa miaka mingi,hivyo alimpongeza Rais Dk.Samia kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo yanayohitajika na kuboresha mazingira.
Kwa upande wake,Msuya amesema mradi huo wa uboreshaji mfumo rahisi wa uondoshaji na kutibu majitaka ya Gereza la Butimba utasaidia kuboresha maji ya Ziwa Victoria na kuyafanya kuwa salama kwa watumiaji.
Meneja miradi wa MWAUWASA,Celestine Mahubi,katika taarifa ya mradi huo amesema umegharimu Euro 856,462.41 (sh.1,969,863,543.00),kwa ufadhili wa Serikali na wabia a maendeleo Benki ya Uwekezaji ya Ulaya(EIB) na Shirik la Maedeleo la Ufaransa (AFD),umezingatia athari za mazingira.
Amesema mradi huo wa miundombinu ya majitaka utaboresha hali ya usafi na mazingira katika Gereza la Butimba ambapo utawanufaisha watu 4,000 wa jamii ya wafungwa na watumishi wa gereza,umekamilika na unatoa huduma ya kuondosha na kutibu majitaka eneo la gereza hilo.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,Peter Bega amesema maji ni agenda ya kwanza ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha wananchi wanayapata.
Amekemea watumishi kero wa MWAUWASA wanaochelewesha wananchi kupata huduma ya maji na kuwataka wabadilike na kuhakikisha maji yanawafikia baada ya mradi wa Matokeo ya Haraka wa Luchelele kukamilika.
“Watumishi wote wakifanya kazi na kuwajibika hakuna sababu ya CCM kukosa kura,yote yakifanyika na kukamilika itakuwa na uhakika wa kupata ushindi wa asilimia 90 katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani,”amesema Bega.
Aidha, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Nyamagana,Witness Makale amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi za miradi ya maji inayolenga kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani, hivyo miundombinu yake itunzwe ikiwemo kudhibiti wanaochezea koki kuchepusha maji kwani dhamira ya Rais kila mtu apate maji.sss