NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Suleiman Mahmoud Jabir(kulia), mara baada ya kuwasili katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akiwa ameshika jezi za Zanzibar Heroes alizopewa zawadi na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Suleiman Mahmoud Jabir(kulia) baada ya kuwasili Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akiwa katika kikao cha pamoja na Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar wakiongozwa na Rais wa Shirikisho hilo.
…………………
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika sekta ya michezo nchini yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Mwinyi.
Kauli hiyo ameitoa wakati akipokea zawadi ya jezi ya Timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes kutoka kwa Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar(ZFF)huko Ofini kwake Afisi Kuu ya CCM Zanzibar iliyopo Kisiwandui Unguja.
Alisema Zanzibar imeanza kuandika historia mpya ya kuingia katika ramani ya nchi za visiwa Barani Afrika ambazo wananchi wake wananufaika na fursa ya michezo mbalimbali hasa mpira wa miguu kutokana na uwekezaji wa miundimbinu bora inayowekwa na Serikali katika sekta ya michezo.
Dkt.Dimwa,alieleza kuwa Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya michezo mbalimbali ili wananchi wote hasa vijana waendeleze vipaji vyao vitakavyowapatia fursa ya kujiajiri wenyewe na kushiriki katika mashindano ya kitaifa,kikanda na kimataifa.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar Dkt.Dimwa, amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Zanzibar inakuwa ni kitovu cha michezo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Wito wangu kwa wananchi wote bila kujali tofauti zetu za kisiasa na kidini tujitokeze kwa wingi kushiriki katika michezo mbalimbali sio tu mpira wa miguu bali tunayo michezo mingi inayoweza kuwa ni sehemu ya ajira na tukapata fedha nyingi kuliko hata watu walioajiriwa serikalini na sehemu zingine.
Tuwe wabunifu na wenye kujituma katika kuhakikisha tunatumia vizuri fursa hii ambayo ni sehemu kubwa ya kipaumbele cha Serikali yetu, na tulinde miundombinu ya michezo ili iweze kudumu zaidi”,Alisema Dkt.Dimwa.
Katika kikao hicho aliwapongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar(ZFF) kwa uchapakazi na ubunifu wao ulioleta mageuzi makubwa nchini na kujenga matumaini mapya kwa mashabiki wa soka hali inayoleta hamasa kwa vijana wengi kujitokeza kuingia katika michezo.
Dkt.Dimwa,alisema kuwa jezi iliyobuniwa na ZFF ina viwango vinavyoendana na ukubwa na hadhi ya timu ya Zanzibar na kwamba wananchi wanatakiwa kwa umoja wao waendelee kuunga mkono juhudi hizo.
Alisema mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 188 inayofafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo,shughuli za utamaduni,sanaa,michezo na ubunifu zitaimarishwa ili kuendelea kuburudisha,kujenga afya na kuzifanya Zanzibar kuwa kituo cha mfano katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuimarisha miundombinu na vituo nvya taaluma za utamaduni,sanaa na michezo, na kukuza vipaji vya wasanii ili kuchukua nafasi maalum katika kujenga uchumi na kuzalisha ajira hasa kwa vijana.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Suleiman Mahmoud Jabir, alisema dhamira ya shirikisho hilo ni kuinua soka la Zanzibar na kufikia katika viwango vya kimataifa vinavyoenda sambamba na malengo ya serikali.
Rais huyo Suleiman, alieleza mpira wa miguu kwa sasa ni biashara na ajira zenye faida kubwa hasa endapo vijana wanapoamua kutumia vipaji vyao vizuri kuhakikisha wanaingia katika soko hilo la ajira kupitia sekta ya michezo.
Pamoja na hayo ameeleza kuwa Shirikisho hilo pamoja na mambo mengine litasimamia ipasavyo sheria na kanuni za mpira wa miguu nchini ili kuhakikisha wachezaji,waamuzi na walimu wanaozalishwa nchini wanakuwa na viwango bora.