Mwandishi wetu, Iringa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Maxmilian Chuhula amewataka wasomi wa vyuo vikuu kutoogopa kufanya tafiti nje ya nchi ili mbali ya kuongeza maarifa, wazijue tabia za watu wengine kwenye mataifa yao.
Dk Chuhula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Historia Tanzania, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachohusu matarajio ya utengamo wa Afrika, mgogoro wa Sahara katika ukumbi wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU).
Kitabu hicho kilicho chapishwa na Africa Proper Education Network (APE), kimeandikwa na Dk Maxmilian akishirikiana na mhadhiri mwingine wa UDSM, James Zotto.
“Fanyeni tafiti nje ya Tanzania mjifunze vitu vingi, mjifunze kuhusu watu wengine wa Afrika na muongeze maarifa,” amesema na kuongeza;
“Kitabu hiki kinao uhalisia na naamini mkikisoma kitawaongezea maarifa ya kutosha kuhusu utengamano wa Afrika hasa mgogoro wa Sahara Magharibi,” amesema.
Alisema kitabu hicho kitakuwa miongoni mwa vitabu vitakavyo wapatia wanafunzi uelewa mpaka kuhusu masuala ya utengamano waAfrika, hasa mgogoro wa Sahara Magharibi.
Dk Chukula alisema licha ya kuwa na maandiko mengi, kitabu hicho ni cha kwanza kwenye safari yao kitaaluma.
Awali Zotto alisema uzinduzi wa kitabu hicho pia unamuenzi Profesa Gaudence Mpangala aliyekuwa kati ya wasomi wachambuzi mahiri kwenye masual ya kisiasa akifundisha RUCU mpaka mauti ilipomfika Februari 4, 2021.
“ Profesa Mpangala ni kati ya wahadhiri walio mjenga kitaaluma hasa katika masuala ya historia na migogoro, alinisimamia na kumuenzi, tukaona tuje kuzindulia kitabu kwenye chuo hiki,” amesema Zotto.
Mwandishi mwingine wa kitabu hicho, Dk Chuhula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Historia Tanzania amesema hakuna ubishi kwamba, ili kuandika vitabu wanafunzi lazima wajikite katika kufanya tafiti.
Awali, Kaimu Mkuu RUDU, DK Makungu Bulayi aliwataka wanafunzi kujenga tabia ya kusoma vitabu na kujikita katika uandishi ili kufikia malengo yao kitaaluma.
Alisema uzinduzi wa kitabu hicho umekiheshimisha chuo chao hasa wakati huu wa utandawazi ambao, wanafunzi wanapaswa kujifunza mambo mengi Zaidi kwa kusoma vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni tofauti.
Baadhi ya wanafunzi wa RUCU, walisema ujio wa kitabu hicho chuoni kwao utawapa mwanga mpana hasa wale waliojikita kwenye masuala ya historia.
“Tumepata mwanga mkubwa sana kwa ujio wa kitabu hiki Zaidi, tumejifunza kwamba tunaweza kufanya tafiti hata nje ya Tanzania,” amesema Daud Daud, mwanafunzi wa RUCU.