*Asisitiza uadilifu na uwajibikaji kwa mali za umma
*Apongeza Serikali Njombe mrejesho kwa wananchi, chama kwa usimamizi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel John Nchimbi, amesema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ndani ya miaka mitatu, ni nyezo inayobeba ukweli wa kutosha kusambaratisha uongo unaoenezwa na baadhi ya wapinzani wa kisiasa kupitia mikusanyiko yao.
Amewataka wana-CCM wote kuendelea kujiamini na kutembea kifua mbele wanapozisema, kuzitangaza na kuikumbusha jamii kuhusu kazi za maendeleo na ustawi wa jamii, zinazofanywa na Serikali za CCM ili wananchi waendelee kuuona ukweli, wakitofautisha na uongo unaoenezwa kwa propaganda nyepesi za kisiasa.
Balozi Nchimbi amesema hayo leo, Aprili 19, 2024, alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wanaCCM wa Mkoa wa Njombe, kupitia Mkutano Maalum wa Mkoa, uliofanyika mjini Njombe.
“Mambo yaliyofanywa na Serikali ndani ya hii miaka mitatu, unaweza kuona kama ni miujiza. Kazi kubwa sana inafanyika. Ni wajibu wetu kuitumia nyenzo yenye ukweli kupambana,” amesema.
Kupitia mkutano huo, ambao Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka aliwasilisha taarifa ya mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, iliyohusisha miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi, Balozi Nchimbi pia amerudia kusisitiza kwa watendaji wa Chama na Serikali ulazima na umuhimu wa kuwa waadilifu wakati wote kwenye masuala yanayohusu rasilimali za umma, kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu.