Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza katika kikao na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kilicholenga kujadili mikakati ya usimamizi wa mazingira na kutoa maelekezo, jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.
Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw.Thobias Mwesiga akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC katika kikao cha mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kilicholenga kujadili mikakati ya usimamizi wa mazingira na kutoa maelekezo, jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.
Sehemu ya washiki wa kikao na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kilicholenga kujadili mikakati ya usimamizi wa mazingira na kutoa maelekezo, jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kilicholenga kujadili mikakati ya usimamizi wa mazingira na kutoa maelekezo, jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.
………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza maafisa mazingira katika halmashauri zote kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira katika maeneo yao.
Ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.
Amesema Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeanishisha wazi kuwa maafisa hao wanapaswa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa mazingira kwa Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC kwa ajili ya ufuatiliaaji.
Aidha, kutokana na changamoto mbalimbali za kimazingira hususan kelele na mitetemo, Dkt. Jafo amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais katika upangaji wa miji.
Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hatua hiyo itasaidia kubaini upangaji bora wa miji hususan katika matumizi ya maeneo husika kuepusha migogoro ya kimazingira.
Halikadhalika, akizungumza na mameneja wa kanda wa NEMC, Waziri Jafo amewahimiza kuongeza kasi ya utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ili mirai iliyokidhi vigezo iweze tekelezwa.
Amesema kuwa si jambo jema kuona wawekezaji hao wanacheleweshewa vyeti ambavyo wameomba kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira ili waanze miradi.
Pamoja na kuwapongeza kwa usimamizi wa sheria katika kanda zao amewataka kukagua shughuli za wawekezaji wa miradi mbalimbali wanaopatiwa vyeti hiyo kama wanafuata sheria.
“Nendeni mkafuatilie kama waliopata vyetu wanatekeleza yale masharti yaliyomo kwenye vyeti hivyo na sio mtu ameweka cheti chake kama kai ya harusi.
“Tunataka kuona taasisi yetu ya NEMC inaendelea kuheshimika kwa kazi nzuri inayofanya hasa katika usimamizi wa mazingira na sisi kwa upande wake tukiwa wasimamizi wa Sera,” amesema.
Amewasisitiza mameneja hao kuwa na utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa uandaaji wa vyeti unavyoendelea na kuwaelekeza wasaidizi wao waongeze kasi ili vitolewe kwa kasi.