……………………
Songea
WAKULIMA wa mahindi mkoani Ruvuma,wamekumbushwa umuhimu wa kufuatilia maendeleo ya mazao yao mashambani na kuhakikisha wanavuma mazao yaliyokomaa ili waweze kupata soko la uhakika na pindi msimu wa ununuzi utakapoanza mwezi Julai.
Wito huo umetolewa jana na Meneja wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA) Kanda ya Songea Zenobius Kahere, wakati akizungumzia maandalizi ya ununuzi wa mahindi katika msimu wa kilimo 2024/2025 ofisini kwake mjini Songea.
Alisema,hatua hiyo itawezesha wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula kupata nafaka bora kwa ajili ya akiba ya chakula kwa wananchi watakaopatwa na upungufu wa chakula katika maeneo yao.
Aidha alisema,katika msimu wa mwaka huu wakala utanunua mahindi kwa kuwahusisha wakulima wakubwa,wafanya biashara wakubwa na wakulima wadogo.
Alisema,wakulima wakubwa waliokusudiwa katika mpango huo ni wakulima wanaoanza na ekari 100 na wenye uwezo wa kuuza tani 200 na kuendelea.
“Kwa upande wa wafanya biashara ni wale wenye uwezo wa kununua mahindi kutoka kwa wakulima kuanzia tani 2,000 hadi 5,000”.
Alisema,vigezo vilivyowekwa kwa wakulima wakubwa watakaotaka kuuza mahindi kwa Serikali ni lazima atoke kwenye Halmashauri anayofanyia shughuli zake za kilimo ili NFRA iweze kumpa mkataba wa kuuza mazao yake kama mkulima na siyo vinginevyo.
Kwa mujibu wa Kahere ni kwamba,wafanyabiashara wakubwa watalazimika kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa Halmashauri ya wilaya wanakofanyia biashara zao ili muda utakapofika wa kuanza kununu nafaka iwe rahisi kwa NFRA kuweka usimamizi mzuri wa upatikanaji wa nafaka hiyo.
Amewataka wakulima na wafanyabiashara wanaotaka kuuza mahindi kwa wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula kutuma maombi yao haraka ofisi ya meneja wa kanda ili kutoa nafasi ya kuanza mchakato wa kupitia maombi yao ambayo mwisho ni tarehe 20 Machi.
Alisema,wakulima ambao hawatahusika katika mpango huo wanatakiwa kuendelea kujiandaa kuuza nafaka hasa mahindi kwenye vituo maalum vitakavyopangwa wakati zoezi la ununuzi litakapoanza.
“kwa hiyo wasiwe na wasiwasi kwamba wamewekwa pembeni hapana,wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula inawatambua na nafasi zao zipo na watapata nafasi ya kuuza nafaka zao kwa serikali kupitia wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula(NFRA)”.
Pia amewataka wakulima, kuhakikisha wakati wa mavuno wanazingatia kanuni muhimu ikiwemo kumwaga mazao kwenye maturubai badala ya kumwaga kwenye vumbi ili kuepuka kuchanganyika na uchafu.
Amewakumbusha wakulima,kuhakikisha wana hifadhi mazao yao kwenye mazingira safi na salama wakati huu wanasubiri kufunguliwa kwa soko.
Mkulima wa mahindi kutoka kijiji cha Matimira Halmashauri ya wilaya Songea Ali Ngonyani,ameiomba serikali kufungua soko mapema ili waweze kupata fedha za kulipa madeni ya pembejeo walizochukua wakati wa mandalizi ya msimu wa kilimo.
John Komba mkulima wa mahindi kutoka kijiji cha Maposeni alisema,kufunguliwa kwa soko mapema itasaidia kudhibiti tabia ya inayofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaokwenda moja kwa moja mashambani.
Alisema kuna wafanyabiashara wana walaghai wakulima kwa kununua mahindi kwa bei ndogo isiyolingana na gharama za uzalishaji.