Mwenyekiti wa CCM Wilayaya Nyamagana, Peter Bega (katikati).leo akizungumza na waandishi wa habari wakati Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo ilipotembelea mradi wa kimkakati wa barabara ya Buhongwa-Igoma, unaojengwa kwa zaidi ya sh. bilioni 22.4.Kulia ni Mwenyekiti wa UWT Nyamagana, Witness Makale na kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo,Amina Makilagi.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi(kushoto),akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Nyamagana ilipotembelea mradi wa kimkakati wa barabara ya Buhongwa-Igoma yenye urefu wa km 14 leo.Mradi huo ni wa uboreshaji wa Majiji na Miji Nchini (TACTIC).
Mshauri wa Mradi wa Barabara ya Buhongwa-Igoma,Jared Kweba akitoa maelezo kwa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Nyamagana, leo ilipotembelea barabara hiyo itakayounganisha barabara kuu za Mara na Shinyanga zinazoanzia katikati ya Jiji la Mwanza.
…………………….
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Nyamagana imeishukia Kampuni ya ukandarasi ya ZHONGMEI Engineering Group ya China, inayojenga kwa kiwango cha lami barabara ya Buhongwa hadi Igoma yenye urefu wa km 14 ikimtaka kuukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba.
“Mradi huu ni kilio cha Nyamagana kwa miaka mingi, ni ahadi iliyotolewa na serikali ya awamu ya nne.Rais Dk.Samia ametoa zaidi ya sh. bilioni 22 na mkandarasi ameshalipwa sh. bilioni 3.409, hatuoni kwa nini mradi unasuasua,tuusimamie na hatutaki excuse (samahani),”amesema.
Bega amewatoa wananchi hofu ya kukosa barabara kuwa itakamilika kwa sababu Rais Dk. Samia alishatoa fedha,kazi ya kusimamia si yake bali ya aliowapa dhamana ili kazi ifanyike kwa wakati na kuleta manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema mradi huo ukikamilika utafungua uchumi wa wananchi wa Nyamagana,ni mtaji wa kisiasa wa CCM na kuonya wanaotaka kuukwamisha wanaikwamisha Serikali na Chama Cha Mapinduzi,usipokamilika na kuusemea,uchaguzi ukifika wapinzani wataunyooshea vidole na kutupunguzia kura.
Mwenyekiti huyo wa CCM Nyamagana amesema haiwezekani kukosa ushindi (kura) sababu ya mtu mmoja kutotimiza wajibu na hakuna sababu ya kumsikiliza mkandarasi,lazima asimamiwe mradi ukamilike kwa wakati.
“Fedha zipo, tunakwama wapi? Ni fedheha msimamizi na mshauri wa mradi kutofautiana lugha.Mradi huu ni ahadi ya serikali ya awamu ya nne pia awamu ya tano,Rais Samia ana imani na ninyi, alishasema ataitekeleza miradi yote kwa wakati,kwa nini tufike 2025.Ajira zipatikane kwa vijana mradi ukopita,”amesema Bega.
Mhandisi wa barabara wa kampuni ya ZHONGMEI Engineering Group,Wang Zhengkai,amesema changamoto ni gharama kubwa zilizowasilishwa na MWAUWASA na TANESCO za kuhamisha miundombinu ya maji na umeme ambapo MWAUWASA iliwasilisha sh.milioni 800 na TANESCO zaidi ya sh.bilioni Moja ilhali fedha zilizotengwa na mradi ni sh. milioni 250 za umeme,maji na simu.
Naye mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ya Siasa,Dk.Kerebe Luteri amesema aliopewa dhamana kwa niaba ya wananchi,wasimamia barabara hiyo ijengwe na kukamilika kwa wakati,haoni hoja ya msingi mradi kuchelewa sababu ya miundombinu ya maji na umeme wakati usanifu na upembuzi yakinifu ulifanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi kwa niaba ya watendaji wa serikali amesema wamepokea maelekezo ya kamati ya siasa na kuahidi kuyafanyia kazi huku akionya wanaotaka kukwamisha mradi huo wa barabara kufanya ubadhirifu na kuiba vifaa wakatafute kazi nyingine.
Awali Mhandisi Jane Mdulla kwa niaba ya Mratibu wa Mradi huo wa TACTIC,Mhandisi Dustan Kishaka,amesema unalenga kujenga uwezo wa mamlaka za serikli za mitaa kujiendesha zenyewe kupitia mapato ya ndani baada ya kuboresha miundombinu wezeshi ya kuvifikia vyanzo mbalimbali vya mapato na utainua uchumi wa Jiji la Mwanza.