Meneja wa TPA Kanda ya zIwa, Erasto Lugenge (kushoto), leo akitoa taarifa ya Mradi wa Uboreshaji na Upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Nyamagana (kulia) walipotembelea mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi (kushoto),akitoa ufafanuzi kuhusu Mradi wa Uboreshaji na Upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wa Wilaya hiyo leo, walipotembelea mradi huo.
Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Uboreshaji na Upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini kupitia kampuni ya M/S Dar Al-Handasah Consultants (Shair and Partners) ya Lebanon,Mhandisi Abraham Msina wa TPA (wa pili kutoka kulia), akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wa Wilaya eneo la gati la bandari linaloboreshwa leo, walipotembelea mradi huo.
Wajumbe wa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wa Wilaya walipotembelea mradi wa uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini wakimsikiliza Mhandisi Abraham Msina wa TPA (wa pili kutoka kulia),leo.
Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Nyamagana, leo ikitoka kukagua miundombinu ya mradi wa uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Wilaya ya Nyamagana imewataka wataalamu na wahandisi kuwasimamia kwa weledi wakandarasi waotekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati wilayani humo ili kazi zifanyike usiku na mchana kuepuka kuongezwa muda.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ilipotembelea kukagua miradi ya kimkakati ukiwemo wa uboreshaji wa bandari ya Mwanza Kaskazini.
Amesema miradi ya kimkakati mikataba kuongezwa muda kinyume cha makubaliano sababu zinakuwa nyingi hivyo CCM hairidhishwi na hatua hiyo kwani wapo wabadhirifu wanaofanya hivyo ili kujinufaisha.
Ameipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Kanda ya Ziwa kwa usimamizi mzuri uliomwezesha mkandarasi kufikisha asilimia 37 ya mradi wa uboreshaji wa bandari,kwa fedha hizo sh. bilioni 18 si ndogo,ili kuiwezesha meli ya MV Mwanzaianze kutoa huduma kwa wananchi kazi ifanyike usiku na mchana gati likamilike kwa wakati.
“Nawapongeza TPA kazi inakwenda vizuri kwa asilimia 37, mradi utakamilika kwa wakati.Tukifanya kwa bidii tutaiheshimisha serikali na CCM na tuna imani kubwa mradi huu utakamilika kwa wakati wananchi wapate huduma na watu wafanye biashara ka kupeleka bidhaa nje na kuleta ndani kutoka nje ya nchi jirani za Kenya na Uganda”amesema Bega.
Mwenyekiti huyo wa CCM amemtaka mkandarasi kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation(CR15G) kufanya kazi usiku ili meli ya MV Mwanza ambayo tayari imekamilika iweze kutia nanga katika Bandari ya Mwanza Kaskazini,kinacholewesha ni uboreshaji wa upanuzi wa bandari hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Aina Makilagi amesema mradi huo ni mzuri unatekelezwa kwa mujibu wa mkataba ambapo Rais Dk.Samia ameendelea kutoa fedha ili mradi huo ukamilike na kuwahudumia wananchi na kuleta manufaa ya kiuchumi na kijamii.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ni agenda ya serikali kuhakikisha inakamilika wananchi wapate huduma ukiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo.
Awali akitoa taarifa ya Mradi huo wa Uboreshaji na Upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini,Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa, Erasto Lugenge, amesema TPA katika mwaka wa fedha 2023/24 ilitenga fedha sh.18,606,443,416.66 kutekeleza mradi huo ambao umefikia asilimia 37 na utakamilika Novemba 2024.
Amesema asilimia hizo 37 zilizofikiwa zinahusisha ujenzi wa maegesho ya meli,miundombinu ya barabara na sakafu ngumu,jengo la abiria na la pampu ya mafuta,miundombinu ya kuhifadhia mafuta na mifereji ya maji.
Kazi zingine ni ujenzi wa jingo la ukaguzi wa abiria na mizigo,uzio wa bandari,kuweka miundombinu ya umeme,kuhamisha miundombinu ya reli na madaraja katika Bandari ya Mwanza Kusini na ujenzi wa kingo za Mto Mirongo.
“Changamoto zinazoathiri utendaji katika Bandari za Ziwa Vitoria ni kina cha maji kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ufinyu wa eneo la shuguli za mradi kutokana na shughuli zisizo za bandari zinazoendeshwa jirani na bandari maeneo ambayo kisheria yanapasa kuwa chini ya usimamizi wa TPA,”amesema Lugenge.
Amesema katika kuchagiza maendeleo kwa wananchi TPA imejipanga kutekeleza mipango mbalimbali ya serikali kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050 na Ilani ya CCM 2020-2025 ili kutumia fursa za jiografia ya Mkoa wa Mwanza.
Lugenge amesema moja ni kuhakikisha mradi wa uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Mwanza Kaskazini unakamilika kwa wakati,kuendelea kutoa huduma kwa watumiaji wa bandari hiyo kipindi chote cha uboreshaji na baadaye.