Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma
“Mtu ni Afya, Jali Afya Yako”, huo ni msemo maarufu unaotumiwa na maofisa wa Wizara ya Afya kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza afya zao kwani afya ni mtaji muhimu katika maisha ya mwanadamu hasa katika kufikia mipango na maendeleo endelevu. Kutokana na umuhimu wa afya bora kwa wananchi, serikali imekuwa ikisisitiza sana wananchi wake kuwa na utaratibu au utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuwa na uhakika wa afya zao, na endapo watagundulika kuwa ni wagonjwa, basi wataanza matibabu mapema ili kudhibiti magonjwa na hivyo kuweka afya zao katika mazingira bora na salama.
Kimsingi, serikali inawajbika moja kwa moja kuhakikisha afya na maisha ya wananchi wake yanakuwa salama. Kutokana na wajibu huu wa serikali kwa wananchi wake, suala la kuwafikishia wananchi huduma bora za afya bila kujali umbali au maeneo wanayoishi halikwepeki.
Ndiyo maana ujenzi na ukarabati wa zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mkoa, na zile za rufaa unaendea nchi nzima. Vilevile, sekta binafsi inashiriki kikamilifu katika kujenga na kuboresha vituo vya afya na hospitali ili kasi ya kuwafikishia wananchi huduma bora iongezeke kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya nchi.
Utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi hauwezi kufanikiwa kama hakutakuwa na raslimaliwatu wa kutosha wa kuhakikishia utoaji wa huduma bora kwa wananchi, ndiyo maana serikali inaendelea na utaratibu wa kuajiri wataalamu wa afya bila kusahau mpango wa kutoa mafunzo na hatimaye kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi popote walipo.
Ikumbukwe kuwa moja ya vipaumbele sita vya kisera vya Wizara ya Afya kwa mwaka 2024/2025 ni pamoja na kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kuwafikishia wananchi huduma bora kule walipo. Januari 31, 2024 kulifanyika Uzinduzi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango alisema katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi kuanzia katika ngazi za chini kabisa, serikali imetenga shilingi bilioni 899.4 kufanikisha azma ya kuwajengea uwezo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wapatao 137, 294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
“Wahudumu wa afya mtakaopewa dhamana ya kutekeleza jukumu hili zingatieni weledi na kujituma pamoja na kutoa rai kwa jamii kupokea mpango huu na kuthamini huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kulinda na kuboresha afya katika jamii,” anasema Dk. Mpango.
Kusudio la serikali la kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ni kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma za afya ili kuimarisha afya za wananchi wote.
Wahudumu hawa watakuwa na jukumu la kutoa elimu ya afya, huduma za afya kinga, huduma tembezi na mkoba na baadhi ya huduma za awali za tiba kabla ya kutoa rufaa. Huduma zote hizi ni msingi mzuri wa kuimarisha afya za wananchi na kuepuka kutumia gharama kubwa kutibu wananchi kwa mambo yanayoepukika kupitia utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anaunga mkono mpango wa kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutokana na umuhimu wao kwani wana mchango mkubwa katika sekta ya afya na wamesaidia sana kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya, kupunguza mzigo kwenye vituo vya afya kwa kuimarisha kinga ya maradhi katika jamii.
“Ukiangalia Ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kila wagonjwa 100, wagonjwa 50 wameibuliwa na watoa huduma wa afya ngazi ya jamii, kwa hiyo watakwenda kupunguza gharama za kuwatibu watu, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wagonjwa wanafikia tatizo likiwa hatua za mwisho, kisukari na matatizo ya figo wagonjwa wanachelewa kubaini matatizo haya,” amesema Ummy.
Kiukweli Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hasssan akisaidiwa na wataalamu wa Wizara ya Afya imejizatiti kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi kwa kuhakikisha inafanikisha mahitaji yote muhimu yanayohitajika kwa watoa huduma hawa yakiwemo masuala ya mafunzo kwa miezi sita darasani na nje ya darasa na vitendea kazi.
Kwa wataofanikiwa kuchaguliwa na hatimaye kuhitimu mafunzo, watakuwa na jukumu la kufikia kaya 25 kwa wiki na kaya 100 kwa mwezi huku wakitakiwa kutoa ripoti kwenye uongozi wa kituo cha afya kilichopo karibu nao chini ya mtendaji wa kata.
Aprili 06, 2024, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi ilitangaza nafasi za kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 8,900 watakaokwenda kutekeleza afua jumuishi za afya, lishe na ustawi wa jamii katika ngazi za vitongoji na vijiji.
Katika tangazo hilo, awamu ya kwanza ya mpango huo utaanza kwenye mikoa 10 na halmashauri mbili kwa kila mkoa na itakayonufaika ni Geita wahudumu 920, Kagera 878, Kigoma 1,094, Lindi 1,724, Mbeya 836, Njombe 746, Pwani 480, Songwe 774, Tabora 966 na Tanga 482. Bada ya kukamilika awamu hii ya kwanza, utekelezaji wa mpango huu utaendelea kwenye mikoa na halmashauri zingine za Tanzania Bara.
Wahudumu wa afya ngazi ya jamii watasambazwa kwenye kila kitongoji au mtaa ambapo kwa kila mtaa au kitongoji kitapata wahudumu wawili yaani mwanaume na mwanamke.
Aidha, hivi karibuni kwenye kikao kifupi baina ya Mawaziri kutoka Wizara za Kisekta na ugeni kutoka nchini Uingereza ukiongozwa na Waziri wa Uingereza na Maendeleo ya Afya Andrew Mitchel, Waziri Ummy akiendelea kusisitiza umuhimu wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
“Mikakati hii ambayo tumeanza nayo ua utoaji wa Elimu ya Lishe pamoja na Uzazi wa Mpango kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili watumike kutoa elimu ya afya hizo kwa wananchi kwa kuwa wao ndio wapo karibu zaidi na wananchi,” amesema Ummy.
Hivyo basi, wahudumu wa afya ngazi ya jamii wahakikishe wanatimiza majukumu yao ipasavyo ili kuendelea kulinda afya za wananchi.
Wahudumu hawa wajue wana deni katika udhibiti wa Magonjwa ya kuambukiza, Kifua Kikuu na Malaria, Magonjwa yasiyoambukiza na Magonjwa ya mlipuko, Masuala ya Afya ya Uzazi, Lishe, Mama na Mtoto na Usafi wa Mazingira. Serikali, wizara na wananchi kwa ujumla tunawategemea wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuwa sehemu ya kuboresha afya za wananchi. Msituangushe tafadhali.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.