Na Sophia Kingimali.
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili(MNH) imepokea mashine ya kisasa ya uchunguzi wa saratani ya matiti kwa wanawake ambayo pia itatumika katika kuwafundishia wataalam na kufanya utafiti.
Pia wanawake wameaswa kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti kuhakikisha wanapata tiba ya haraka pindi wanapogundulika na tatizo hilo kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
Akizungumza leo wakati wa mapokezi ya mashine hiyo Dkt Hamad Nyembea wakati akimuwakilisha waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Takwimu za kidunia zinaonyesha wanawake milion 2.3 wanahundulika kuwa na saratani ya matiti kila mwaka.
“Tafiti za kidunia zinaonyesha wanawake milioni 2.3 wanagundulika na saratani ya matiti kila mwaka lakini hapa nchini wanawake 42,000 kila mwaka wanagundulika na saratani hiyo huku wanaofika kwenye vituo vya afya kupata matibabu ni asilimia 38 tu”,Amesema Nyembea.
Amesema kupokea kwa mashine hiyo ambayo ni ya kwanza nchini yenye kutoa huduma za kibobezi itasaidia kurahisisha utoaji wa huduma hiyo.
“Hii sio kuwa ni mashine ya kwanza ya kupimia saratani ya matiti tayari mashine zipo katika hospitali zetu ila hii ni ya kwanza nchini yenye kufanya huduma za kibobeze kwani inaweza kupima,kupiga picha 3D na kubaini chembechembe za saratani lakini pia inafanya utafiti,”amesema.
Amesema ujio wa mashine hiyo unaonyesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani kwani unawezesha kukuwa kwa teknolojia katika sekta ya afya.
Adha Dkt Nyembea amesema saratani ambayo kwa sasa inaisumbua nchi ni saratani ya shingo ya kizazi na tayari jitahada zinaendelea kufanyika ila kuhakikisha saratani hiyo inaisha nchini.
Sambamba na hayo ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika sekta hiyo huku akitoa rai kwa watendaji kuhakikisha wanaitunza mashine hiyo na kuhakikisha inafanya kazi iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospital ya Taifa ya Muhimbili Profesa Mohamed Janabi amesema mashine hiyo imegharimu milioni 800 hii ni ya kwanza nchini kwani itasaidia kuliona ziwa kwa 3D.
Amesema sasa hivi huduma zote ikiwemo kipimo cha MRI hivyo itampunguzia mgonjwa kutoka kwenda kupima badala yake vyote vinafanyika kwenye chumba kimoja.
Amesema saratani ya ziwa inatokana na ulaji hivyo ni vyema kuzingatia ulaji ili kujikinga na saratani hiyo
“Tunajua saratani ya mapafu mara nyingi utokea kwa sababu ya uvutaji wa sigira lakini saratani ya ziwa na saratani ya utumbo mkubwa zinahusiana sana na ulaji wa chakula hivyo tunasisitiza kwenye kinga kuliko tiba kwani tiba inagharama kubwa,”amesema Janabi.
Nae,Muwakilishi wa kitengo cha biashara kutoka GE healthcare Guillaume Fusari amesema ukosefu wa elimu kuhusu saratani ya matiti ndio unapelekea ongezeko la ugonjwa huo ambapo unapelekea vifo hivyo ni muhimu kuwawezesha wanawake ili kupunguza idadi ya vifo.
“Ukosefu wa elimu ndio sababu ya wanawake kuugua ugonjwa huu wa saratani ndio maana kuna umuhimu wa kuwawezesha wanawake ni muhimu ili kuboresha kiwango cha vifo”,Amesema.