OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu utakaoanza Julai, 2024.
Akiwasilisha bungeni utekelezaji wa bajeti ya Mwaka 2023/24 na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa Mwaka 2024/25, Mhe. Mchengerwa mikopo hiyo itaanza kwa utaratibu wa kutumia benki kwa halmashauri 10 za majaribio ambazo ni Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma Ujiji na Songea, Miji ya Newala na Mbulu, Wilaya za Siha, Nkasi, Itilima na Bumbuli.
Aidha, amesema halmashauri 174 zilizobaki zitatumia utaratibu ulioboreshwa ili kuondoa mapungufu yaliyosababisha changamoto za awali kwa kufanya mambo yafuatayo; uanzishwaji wa kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata.
“Majukumu ya kamati ngazi ya kata ni kutambua waombaji na kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha kwenye kamati ya halmashauri, kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kusanifu na kujenga mfumo mpya unaoitwa Wezesha Portal utakaotumika kwa ajili ya taratibu za ukopeshwaji wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, mfumo huu utaondoa changamoto za mfumo zilizokuwepo awali kabla ya mikopo kusimamishwa,”amesema.
Amesema maboresho mengine yaliyopangwa kufanyika ni kujenga uwezo kwa wasimamizi wa mikopo hiyo kwa kuongeza idadi ya 91 wasimamizi wa mikopo kwenye ngazi ya kata ambapo maafisa maendeleo ya jamii 787 wameajiriwa na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu. Watumishi hao na timu nzima itakayosimamia mikopo hiyo katika ngazi zote itapatiwa mafunzo na wataalamu wabobezi wa usimamizi wa mikopo ya aina hiyo.
Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kurekebisha sheria inayosimamia mikopo hiyo na kanuni zake ili kuongeza ufanisi. Baada ya kipindi cha mpito, tathmini itafanyika ili kubaini mfumo bora utakaotumika katika utoaji wa mikopo hiyo.
“Mikopo inayotarajiwa kutolewa ni sh. Bilioni 227.96 ambapo Sh. bilioni 63.67 ni fedha za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa, sh. bilioni 63.24 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na sh. bilioni 101.05 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25.