Na Prisca Libaga Arusha
Shule tatu za msingi zilizoko wilaya ya Monduli zimepewa jumla ya madawati 130 kwa ajili ya wanafunzi 390 zenye thamani ya shilingi milioni 15.
Madawati hayo yametolewa kwa shule za Msingi za Sokoine na Ngarash kila moja ikipewa madawati 50 huku Orarash wakipewa madawati 30 ni kwa ajili ya kupunguza changamoto ya wanafunzi kusoma
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Meneja wa NMB kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa Benki yao imeamua kutoa msaada huo kwa shule hizo Ili kumsaidia Rais Samia Suluhu kupunguza changamoto ndogondogo za Kielimu zinazokwamisha maendeleo ya Elimu nchini.
Amesema Kuwa, katika faida wanayoipata wameamua kurudisha kwa jamii kwenye sekta nne za Afya, Elimu, Mazingira na kusaidia kurejesha au kutoa mkono wa pole kwa majanga mbalimbali yanayotokea nchini.
“kama benki tunapokea maombi mengi, na Kwenye sekta ya Elimu tulipokea maombi ya madawati kwa shule hizi za kifugaji tukaguswa na watoto hawa na leo tumekuja kugawa madawati haya 130 kwa shule tatu ikiwa na gharama ya zaidi ya Sh. 15 Milioni” alisema kuongeza..
“Ombi letu ni mkatunze ili ilete manufaa kwenu ya mda mrefu lakini pia itimize malengo yetu ya kusaidia jamii na kuisaidia serikali kutimiza malengo yake kwenye sekta ya Elimu kwa kupunguza baadhi ya changamoto ndogondogo zinazokwamisha ufaulu mashuleni”.
Diwani wa Meserani Lotha Tarakwa akimwakilisha mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, alisema kuwa wilaya ya Monduli iliyokuwa na upungufu wa madawati 1214, kwa msaada huo wa NMB wa madawati 130, sasa wanaomba wadau wengine wajitokeze kusaidia idadi ya madawati 1084 yaliyobakia.
“Mbali na hilo tuna upungufu wa madarasa 282 na matundu ya vyoo 887 hivyo kwa benki yetu walipoguswa kutoa msaada huu basi wajue bado tuna uhitaji na hatufungi milango kwa wakati mwingine”.
Akizungumza kwa niaba ya Walimu wakuu waliopewa madawati hayo, Mkuu wa shule ya Sokoine, Abdallah Hoza amesema kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 570 walikuwa na upungufu wa madawati 70 kwa ajili ya wanafunzi 210, hivyo msaada huo umesaidia wanafunzi wengi kupata sehemu ya kukalia na itaongeza ufaulu kwa asilimia 60.
Alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo kwa sasa ni baadhi ya wazazi kushidwa kuchangia chakula cha wanafunzi wao, lakini pia kukataa kuwalipia nauli ya usafiri kwa wale wanaotoka mbali na kuhatarisha maisha yao kwa wanyama wakali lakini pia mafuriko hasa kipindi hiki cha mvua.
“Mbali na hayo pia tuna changamoto kubwa ya ubovu wa barabara ya mita 600 inayoingia shuleni ambayo imejaa matope na mashimo, lakini pia tuna shida ya maji hapa shuleni, hivyo tunaomba tuvutiwe maji lakini pia matenki ya utunzaji wa maji tunayovuna hasa kipindi hiki cha Mvua” alisema Hoza.
Kwa upande wake M’bunge wa Monduli, Fredrick Lowassa ameishukuru NMB kwa msaada huo kwa shule za serikali ambazo zitabaki kama tunu kwao.
“Changamoto nimezisikia na naenda kuyafanyia kazi hasa barabara hii mbovu nimeiona lakini kwa sasa nitatoa matanki mawili ya lita 5000 kila moja kwa ajili ya kutunza maji mnayovuna kwenye mvua”alisema Lowassa.
Akipokea msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Afisa Tawala Monduli, Anaeli Mbise amesema kuwa serikali imepokea madawati hayo kwa mikono miwili na wanashukuru kwa sapoti kubwa ambayo wamekuwa wakiipata kutoka kwa benki hiyo nchini.
“Si haya madawati tu, kiukweli NMB mmekuwa karibu na serikali kwa nafasi kubwa sana hasa katika miradi mbalimbali ya elimu na Afya, hakika nawapongeza sana na tunawaahidi ushirikiano wa asilimia 100 kutimiza malengo yenu ya mapato ili kuendelea kutusapoti” alisema Mbise.
Aliwataka wanafunzi na walimu kutunza madawati hayo ili yatumike kwa mda mrefu huku akiwaagiza viongozi wa kata na mitaa kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule au wanafunzi wanahudhuria shule.