Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha wilayani Ludewa mkoani Njombe na kuleta athari kwa baadhi ya vijiji ikiwemo kijiji cha Lihugai kilichopo kata ya Luilo, Mbunge wa jimbo la Ludewa Joesph Kamonga ametoa fedha kiasi cha Sh. Mil. 2 kwa wakazi wa kijiji cha Lihugai ili ziweze kuwasaidia.
Fedha hizo ziliwasilishwa na katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo Gervas Ndaki akiwa sambamba na katibu siasa na Uenezi wa Wilaya hiyo Bi. Shukrani Kawogo kwa niaba ya mbunge huyo.
“ Awali Mbunge alikuja hapa na baadhi yenu mlionana nae na viongozi tuliowakuta hapa tuliwaambia tathmini ifanyike alafu mheshiwa mbunge ataona mahala gani aweze kuwashika mkono, tunashukuru viongozi wenu mwenyekiti wenu wa kitongoji, mwenykiti wenu wa kijiji pamoja na viongozi wetu wa chama wa tawi hili kazi wameifanya, orodha wameiandika tunayo sasa tukaona ni vyema sasa tuweze kufika kuongea nanyi”, Amesema Ndaki.
Amesema Mbunge tayari amesha toa taarifa bungeni juu ya maafa yaliyowapata hivyo kwa sasa wanapaswa kuishi kwa tahadhari juu ya athari zilizotokea hasa katika matumizi ya maji wanapaswa kuchemsha kwani yanapotokea mafuriko maji huingia takataka za aina nyingi ikiwemo vinyesi hivyo ni rahisi kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
Aidha kwa upande wake Katibu siasa na Uenezi wilaya ya Ludewa Bi. Shukrani Kawogo amewapa pole waathirika hao huku akiwataka baadhi ya wananchi hao ambao mazao yao yamesalia yakiwa yameharibiwa na maji kutoyaacha mazao shambani yaliyoharibiwa kwani wanaweza yavuna na kuyatumia kama chakula cha mifugo.
“Haya mazao yaliyo angushwa na mafuriko msiyaache nayo bado yanathamani kwani mnaweza yavuna na kuyauza ama kutumia ninyi wenyewe kama chakula cha mifugo badala ya kuyaacha shambani yakioza”.
Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho wamemshukuru mbunge wao kwa msaada huo alioutoa huku wakiiomba serikali kuendelea kuwasaidia kwani mashamba yao yamesombwa na maji na baadhi ya wananchi hawana sehemu za kuishi kutokana na mafuriko hayo kuharibu nyumba zao.