KUISHI NI KUJIFUNZA
WATANZANIA NA MITANDAO YA KIJAMII..
– Kama Zidane Angeyapuuzia Matusi Ya Materazzi..
Mwanafalsafa Mjerumani, Max Scheler kuna wakati alisema; kwamba wanadamu tuna uwezo wa kudhibiti kila kitu, lakini si sisi wenyewe, kwa maana ya wanadamu.
Na Wahenga wetu walisema; kiumbe mzito.
Ndio, kimoja tu ambacho wanadamu tuna hakika nacho kwenye maisha yetu ni kuwa iko siku tutakufa.
Mengine yote hutokea pengine hata kutarajiwa. Hupita, na mengine mapya huja. Nayo hupita pia.
Sisi watu wa mpira, duniani kote, tunacho cha pamoja; kuwa tuna mapenzi na mpira ule wa duara. Ndio wenye kutuunganisha. Watu wa mpira kwa asili hatuna chuki endelevu. Kama ni kuchukia jambo huchukia kwa muda tu, halafu maisha huendelea.
Zinedine Zidane alitukanwa tusi baya sana na Materrezi, lakini, ukafika wakati wawili hao walikaa meza moja mgahawani. Walikula, kunywa na kuzungumza kirafiki kama wanafamilia ya mpira. Zidanne alimsamehe Materazzi.
Nini kilimtokea Zidanne?
Sisi watu wa mpira tunaukumbuka vema mwaka ule wa 2006. Zilikuwa ni Fainali za Kombe la Dunia. Zinedine Zidane ‘ Zizou’ alikuwa kwenye upeo wa ubora wake.
Alikuwa tayari ameshatimiza miongo miwili kwenye soka akiwa na mafanikio makubwa.
Klabu yake, Real Madrid, msimu wa nyuma yake ilivuna taji la ubingwa wa La Liga. Zidane akaitangazia dunia ya soka, kuwa Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006, zingekuwa za mwisho kwake.
Kwamba angestaafu soka. Na ikumbukwe, fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1998 Zidane aliiongoza Ufaransa kunyakua ubingwa. Ni kwenye fainali hizo, Zidane alitajwa kuwa mchezaji bora.
Hiyo ilikuwa timu ya Taifa ya Ufaransa ambayo ilijaa nyota Wafaransa wasio na asili ya Ufaransa. Kuna Wafaransa walionyesha waziwazi chuki za kibaguzi. Zidane alichukiwa pia. Si kwa jinsia yake, bali kwa rangi yake.
Kwenye Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2006, Ufaransa ilianza vibaya kwa mechi za hatua za mwanzoni. Lakini, Zidane kama nahodha, aliibeba Ufaransa hata ikang’ara kila hatua zilizofuata. Wakafika fainali dhidi ya Italia.
Kwenye mechi ile ya fainali, ambayo Zidane alishaitangaza kuwa ingekuwa ya mwisho kwenye maisha yake ya mpira, Zidane alifunga goli la kuongoza kunako dakika ya saba tu ya mchezo. Ni kwa njia ya penalti.
Zidane akawa pia karibu afunge bao mwanzoni mwa dakika za nyongeza baada ya dakika tisini kwisha.
Lakini, tunachokumbuka leo sisi watu wa mpira, ni kile kilichomtokea Zidane dakika kumi kabla kumalizika kwa dakika 120 za mchezo.
Ilikuwa dakika ile ya 104 pale Buffon, kipa wa Italia, alipookoa mpira wa kichwa wa Zidane ulioonekana unakwenda kutinga wavuni na hivyo kuamua hatma ya mechi.
Dakika kadhaa baadae, tulimwona Zidane akikimbia taratibu kurudi kwenye goli la Italia akimwelekea beki Marco Materazzi, ni beki maarufu kwa rafu zake.
Tulimwona Zidane akimrukia kichwa cha kifuani Materazzi. Naye Materazzi akajiangusha hapo hapo na kulala chali.
Refa alimyooshea Zidane kadi nyekundu. Ukawa mwisho wa Zidane. Tulimwona Zidane, bila kulalamika kwa refa, akitoka taratibu nje ya uwanja huku akiinamisha kichwa. Likawa ndio tukio la mwisho la Zidane uwanjani. Ndilo analokumbukwa nalo.
Inasemwa, Materrazi, kwa lengo la kumtoa Zidane mchezoni, alimtusi Zidane. Lilikuwa ni tusi baya sana kwa mila na desturi za watu wa asili ya Zidane. Kwa asili, Zidane anatokea Algeria.
Kuna jamii duniani, ni vigumu kwa mwanamme kukubali mwanamme mwenzake kumtukania tusi la nguoni kumhusu dada, au mama yake.
Nini adili ya kisa hiki?
Tunajifunza, kuwa Zidane, kwenye soka, alikuwa na hadithi, sio tu nzuri ya watu kuja kusimulia baada ya kuondoka duniani, lakini, alikuwa na hadithi tamu iliyoondolewa utamu wake kwenye dakika ile ya 104 ya mchezo.
Fikiri kama Zidane angeingiwa na ujasiri wa kupuuzia matusi ya Materrazi. Yumkini angebaki na hadithi nzuri na tamu. Kwa tendo lile, kuna waliosahau makubwa yote aliyofanya Zidane kwenye soka, wanakumbuka tukio lile tu.
Hivyo, tunashuhudia, hata kwenye jamii yetu ya Watanzania kwenye mitandao, kuna ambao hutumia vibaya mitandao hiyo na hata kutapika lugha za matusi ili kuwatoa wenzao ‘ michezoni’. Ni kwa maana watu hao huwa na malengo ya kuwanyamazisha na kuwakatisha tamaa wenzao. Wanawake mitandaoni ni wahanga wakubwa wa mbinu hizi.
Na ilivyo, mwanadamu anayekutisha umwogope, ukimwonyesha kuwa humwogopi hata chembe, basi, ataanza kukuogopa wewe.
Akikutukana mpuuze, akirudia kukutukana mpuuze tena, na tena. Endelea na majukumu yako.
Watu hao waliojaza maghala kwa magunia ya matusi wapo, na wataendelea kuwepo kwenye dunia hii. Kisayansi ni wanadamu wenye hisia kali zenye kuwapa hali za kuwa na hofu, majuto, hisia za kufanya uchokozi na kuwa wenye hasira ( Visirani).
Vyote hivyo hupelekea mwanadamu aliye kwenye hali hiyo kujisikia mawili haya; kukimbia, au kupambana. Mababu zetu zamani wakiwa kwenye hali hizo, waliweza porini kumkimbia mnyama au kupambana nae. Hivyo hivyo walipojikuta kwenye vita vya kikabila.
Hisia hizo kali, wataalam wanatwambia hutokea kwenye sehemu ndogo sana ya ubongo wa mwanadamu iitwayo ‘ amygdala’.
Ni ndogo lakini ina umuhimu sana kwenye kuzalisha hisia hizo tajwa. Ni pamoja na kuchochea stress na adrenalin zinazotufanya wanadamu wakati mwingine kufanya maamuzi ya haraka bila kufikiri athari zake.
Zidane yumkini kuwa na kiwango cha juu cha adrenalin na stress ya mchezo, na kwenye dakika za mwisho, mara tu baada ya kukosa goli, matusi yale ya beki Materrazi, yalimfanya afikie ukomo wa ustahimilivu. Inasemwa kitaalam, kuwa katika hali hizo, kiwango cha mwanadamu cha IQ hushuka, na hata uwezo wake wa utambuzi ( Cognitive ability), hupungua.
Hivyo, inapohusu Watanzania na mitandao ya kijamii, izingatiwe, kuwa mengine, ikiwamo matusi yanayofurumishwa na wanadamu wenzetu humo mitandaoni, yumkini ni matokeo ya wahusika kuwa kwenye hali zenye kuwahitaji kutafuta msaada ili waondokane nazo. Na namna mojawapo ya kusaidia ni kuyapuuza matusi.
Mwanadamu usihangaike kumjibu anayekutukana, mjibu anayejenga hoja dhidi yako, kwa hoja, si kwa matusi.
Kuishi Ni Kujifunza.
Maggid Mjengwa.