Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya Akizungumza leo April 15, 2024 jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mafao House Ilala.
Afisa Uhusiano Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Sabato Kusudi akifafanua baadhi ya mambo katika kikao kazi kati ya Ofisi hiyo, Shirika la Viwango TBS na Jukwaa la Wahariri TEF kilichofanyika leo Ukumbi wa Mafao House Ilala jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athuman Ngenya pamoja na viongozi wenzake wa TBS wakichukua maswali yaliyokuwa yaliulizwa na Wahariri baada ya mawasilisho ya mada katika Kikaokazi hicho.
…………………….
NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika kipindi cha miaka mitatu limefanikiwa kwa asilimia 99 kufanya ukaguzi wa shehena za bidhaa 100,851 kabla ya kuingia nchini kwenye lengo la kukagua shehena 100,283.
Akizungumza leo April 15, 2024 jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi cha Ofisi ya Msajili wa Hazina na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mafao House, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Athumani Ngenya amesema kuwa jumla ya bidhaa 151, 570 zilikaguliwa baada yakufika nchini sawa na asilimia 77 la lengo la kukagua bidhaa 197, 415.
“Kuna bidhaa zinafanyiwa utafiti kabla ya kuingia nchini ambapo kuna makampuni ya kimataifa kutoka nchi mbalimbali duniani inafanya kazi ya kukagu ili kujua kama zimekidhi ubora unaotakiwa“ amsema Dkt. Ngenya.
Dkt. Ngenya amesema kuwa mfumo wa ukaguzi uliopo umesaidia kuleta tija katika kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakuwa rafiki kwa ajili ya matumizi mbalimbali nchini.
‘‘Kuna ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kupitia mifumo rasmi, ambapo zinakaguliwa kabla ya kuwasili nchini kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo China na Marekani“ amesema Dkt. Ngenya.
Ameeleza kuwa TBS imeendelea kutoa mafunzo ya ujasiliamali kwa wafanyabiashara wadogo na wazalishaji wa bidhaa ili kuwa salama wa bidhaa na kukidhi ushindani wa soko la ndani na kimataifa.
Dkt. Ngenya amesema kuwa shirika limeaandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote nchini ili kuhakikisha vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya leseni zenye ubora 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji wa viwanda.