Na Sophia Kingimali.
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara nchini Uturuki kwa lengo la kukuza uhusiano wa kideplomasia ya siasa, uchumi, na biashara kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza leo Aprili, 15, 2024 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Rais Dk,Samia anafanya ziara hiyo baada ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan kumpa mwaliko wa kutembelea nchini humo.
Amesema ziara hiyo ni
kubwa na ya kihistoria nchini
kwetu ambayo itaanza April 17 hadi Aprili 21 mwaka huu.
“Nchi ya Uturuki ni moja nchi
ipo kwenye kundi la nchi 20
wanaofanya vizuri hivyo
tunajua ziara hiyo itakuwa ya
kimkakati nchini kwetu,”amesema Makamba.
Ameeleza kuwa lengo lingine la kufanya ziara hiyo ni kupata mtaji na teknolojia ambao nchi ya Uturuki wanayo , kupata masoko ya bidhaa ambayo yapo nchini humo na kupata wawekezaji kwa lengo la kuwekeza nchini.
Amesema tayari wameshaona makampuni makubwa kutoka Uturuki wakifanya shughuli mbalimbali hapa nchini.
Aidha amesema nchi ya Uturuki inasaidia nchi yetu katika kuleta chanzo cha maendeleo kwenye sekta ya elimu afya,na maji.
Makamba amesema Rais Dk. Samia atafanya mazungumzo ya Kiserikali na Rais wa Uturuki na baadae watafanya mazungumzo ya pamoja na wajumbe wa pande zote mbili lengo ni kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano.
Amesema miaka 14 iliyopita Rais aliyekuwepo madarakani alifanya ziara nchini humo na Rais wa Uturuki alikuja nchini mwaka 2017 hivyo kuna uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
“Tuna uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia tangu mwaka 1963 huku tukiwa tumefungua ubalozi wetu mwaka 1979 baadae ubalozi huo ulifungwa mwaka 1984 kutokana na changamoto mbalimbali na baadae waliufungua tena mwaka 2009.
“Sisi tulikuwa na ubalozi nchini Uturuki uliofunguliwa mwaka 2017hapo utaona kuwa uhusiano wetu ni mzuri kwa muda mrefu,”amesema Waziri Makamba.
Amesema Nchi ya Uturuki imekuwa haraka kiuchumi na ni nchi iliyopata maendeleo haraka kwa sababu imeweka mahusiano na nchi za Kiafrika ikiwemo nchi yetu.
“Tunajua kuna wafanyabiashara wengi wanakwenda nchini Uturuki kununua biashara na sisi tunauza huko bidhaa zetu,”amesema.