Kila tarehe 12/04 ni Siku ya Kimaitafa ya Mtoto wa Mtaani Duniani. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini tarehe 15.04.2024 kwa kushirikiana na Makao ya Kulea Watoto wa Mtaani (Amani Center for Street Children) na Wadau wengine washiriki wameadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa watoto wa mtaani zaidi ya 150 katika Makao yao yaliyopo Kaloleni jijini Arusha.
Watoto wa mtaani ni kundi ambalo lipo katika hatari ya kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya. Pia, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ni makubwa kwa watoto hao sababu hawana watu wa karibu wa kuwaangalia na kuwapatia msaada.
Jeshi la Polisi, Watumishi wa Kituo cha Amani Center, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Arusha Mjini, Afisa Maendeleo ya Jamii-Kata ya Kaloleni, Viongozi wa Dini, Watoto wa Mtaani wa Makao na Walio Nje ya Makao na Waandishi wa Habari ni miongoni mwa Wadau muhimu walioshiriki katika maadhimisho hayo.
Kauli Mbiu ya Mwaka huu ni:
KUWAOKOA WATOTO MTAANI NI JUKUMU LETU SOTE, TUWAJIBIKE.
DCEA Kanda ya Kaskazini itaendelea kutoa elimu ya madhara na tatizo la dawa za kulevya katika makundi mbalimbali katika jamii likiwemo kundi hili muhimu la watoto waliopo katika hatari ya kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.