Uchambuzi Wa Habari:
Kwanini Iran Imeishambulia Israel…?
Ilisubiriwa. Ishara zote zilionyesha ingetokea. Taa nyekundu kumulikia hatari inayokuja zilionekana.
Kwamba ingetokea usiku wa kuamkia Jumapili wengi hatukulijua. Ni Wairan wenyewe waliojua. Tumeona, ndege za Iran 300 zisizo na rubani nyingine zikifika kwenye anga ya Israel na kusababisha taharuki kwa raia. Makombora ya balistiki ya Iran yapatayo 200 pia yamerushwa.
Tumeona ‘ Ustaarabu’ pia, kwamba operesheni imefanywa usiku kuepusha madhara kwa raia ikiwamo watoto endapo ingetokea mchana.
Naam, Iran imetangaza kumaliza operesheni yake ya ‘ Kutimiza Ahadi’. Iliahidi kulipiza kisasi.
Kisasi cha nini?
Wiki mbili zilizopita, April Mosi, Ubalozi mdogo wa Iran jijini Damascus, Syria ulishambuliwa kwa makombora. Maofisa kumi wa Ubalozi akiwemo kamanda wa cheo cha juu cha jeshi wa Iran waliuawa.
Iran mara moja iliwatuhumu Waisrael kuhusika. Israel, kama ilivyotarajiwa, hawakukubali, na wala hawakukataa kuhusika. Kwa wachambuzi wa habari wanajua nini tafsiri ya hali hiyo.
Iran ikaahidi kulipiza kisasi. Ayatollah Khomeini mwenyewe akatangaza kulipa kisasi. Inashangaza, hata mara hii, Benjamin Netanyahu ameonekana kushtukizwa kama ilivyotokea kwa Hamas, Oktoba 7.
Iran na Israel ni ‘mahasimu wa jadi’. Tangu mwaka 1979 mahasimu hawa wameishi katika hali ya kusubiri vita vya moja kwa moja kati yao.
Kabla ya jana mahasimu hawa wamekuwa wakipigana kupitia ‘
Mawakala’- Proxy war. Iran imekuwa ikiwatumia wapiganaji wa Hezbollah kule Lebanon. Imewatumia pia wanamgambo wa Huthi kule Yemen, alikadhalika Hamas. Iran imekuwa pia na vikundi vya wanamgambo inavyovisaidia ndani ya Iraq na Syria.
Je, nini kinafuata?
Iran imeshatamka kumaliza kisasi, lakini, yumkini Israel ina kisasi kipya cha kulipa dhidi ya Iran. Marekani imempigia magoti mshirika wake Israel isifanye hivyo.
Netanyahu atataka ‘ kunusuru sura’. Hata asipolipiza kisasi kikubwa, lakini japo ‘ Kakisasi kadogo’!
Hofu iliyopo ni ukweli kuwa kwenye mgogoro kama huu hakuna kisasi kidogo.
Kuna hofu ya ‘ escalation’- kupanuka kwa mgogoro na kuziingiza nchi nyingine, endapo Israel italipiza kisasi.
Na Iran sasa imeona inaweza kupimana ubavu na Israel ambayo, kwa jicho la Iran, ‘ imedhoofu’ kidogo kutokana na Vita vya Gaza na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa Hezbollah.
Je, hili litapelekea Vita Vya Tatu vya Dunia?
La hasha, hofu hiyo ingali mbali kwa vile hata washirika wa Israel, ikiwamo Marekani, hawatokubali, mgogoro huu kati ya mataifa ambalo moja lina nguvu za nyuklia, ukomae sana na kufika mbali.
Maggid Mjengwa.