Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa
Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,
akikagua banda la Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi Mkoa
wa Mjini Magharibi leo Aprili 14, 2024.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.
Selemani Jafo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian
Luhemeja na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
…………………………..
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kwenye nyanja zote za maendeleo, kisiasa, Uchumi, utamaduni
na huduma za jamii yameipatia nchi heshima kubwa kwenye Jumuiya ya
Kimataifa.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo viwanja vya maonesho ya biashara Nyamanzi
Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi wakati wa uzinduzi wa Sherehe
za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema, kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano huo, Tanzania imeendelea
kubaki kwenye historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na
duniani kote kutokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano
viliyoasisiwa na viongozi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao
waasisi wa Muungano huo.
“Tunaposherekea miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, tuna wajibu wa
kujipongeza kwa mafanikio makubwa nchi yetu iliyoyafikia kwenye nyanja zote za
maendeleo kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii. Alisifu Dk. Mwinyi.
Alieleza dhamira ya dhati kwa viongozi mbalimbali walioshika nyadhifa za uongozi
kwa awamu tofauti kwa Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kuendeleza maono ya Waasisi wa Taifa hili kumefanikisha
kudumisha na kuimarisha Muungano huo.
“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina
yetu kwa shughuli mbalimbali za maendeleo umeongezeka na amani ya nchi yetu
inaendelea kudumu” Alisifu Rais Dk. Mwinyi.
Akizungumzia changamoto za Muungano, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
zimeendelea kuchukua hatua madhubuti kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote za
Muungano huo, ikiwemo kuunda Tume na Kamati kwa ajili ya kushughulikia hoja
za Muungano.
Alisema, miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni pamoja na Kamati ya Pamoja ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.
Alisema tangu mwaka huo hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokelewa na
kujadiliwa, kati ya hoja hizo alieleza hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa
kwenye orodha ya hoja za Muungano.
Aidha, hoja zilizobaki Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa zipo kwenye hatua
mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi.
Dk. Mwinyi pia alieleza Imani yake na kwa utashi wa dhamira ya dhati ya Serikali
za pande zote mbili kwamba hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.